NA TIGANYA VINCENT, TABORA
SERIKALI Wilayani Uyui imesema
inakusudia kuendesha Kampeni maalumu ya Nishike
Mkono Mwezi Machi mwaka huu kwa lengo la kukusanya shilingi bilioni 1.5
(1,500,000,000/-) ambazo zitasaidia ujenzi
wa dahari(hosteli) 15 kwenye Sekondari 15 za Kata ili kuwalinda watoto wa kike
na mimba na ndoa za utotoni.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Uyui Gift Msuya wakati akifungua mafunzo ya
siku mbili kwa mama wadogo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tabora-Uyui
yaliandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuwajengea uwezo watoto wa kike ambao
walikubwa na tatizo la mimba za utotoni.
Alisema lengo la kujenga daharia hizo ni kuwaepusha
wanafunzi wa kike wa shule za Sekondari na mimba, vishawishi vinavyowafanya
washindwe kuendelea na shule na kuozeshwa na wazazi wao , kuwapa utulivu wa
kujisomea kwa kuwa karibu na mazingira ya shule na kuwaepusha kuacha shule kwa
sababu ya kutembea umbali mrefu wa kwenda shule ambapo wakati mwingine
wanakutana na matatizo ya kutaka kubakwa.
Mkuu huyo wa Wilaya hiyo alisema kuwa kukamilika kwa
Daharia hizo sio tu kutasaidia watoto wa Kata husika bali wale wanaotoka Kata
jirani ambazo hazina Sekondari ambapo wanafunzi wao wanatembelea umbali mrefu
kwenda jirani.
Aidha Msuya alisema mafunzo hayo ni muhimu sana kwa vijana ili
wapate elimu kuhusu mambo mbalimbali ikiwemo malezi na familia, afya ya lishe ,
ujasirimali, kilimo biashara , uongozi , taratibu za uundwaji wa vikundi vya
uzalishaji mali na fursa za uwezeshaji wa vijana kiuchumi.
Aliwataka mama wadogo hao kutumia fursa waliyopata ya
kupata mafunzo ili kujiendeleza wenyewe na kueneza elimu waliyopata kwa mama
wadogo ambao hawakupata ya kupata elimu hiyo.
Msuya alitaja Kata ambapo daharia zitakazojengwa ni Magiri
, Igalula, Goweko, Usagari, Ilolanguru, Lutende, Mabama, Shitage, Upuge,
Ikongoro, Makazi, Tura , Isikizya na Loya.
Naye Kaimu
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana Julius Toneshi alisema mafunzo hayo
ni kitaifa ambayo yanalenga kuwawezesha mama wadogo kupata mbinu na stadi za
kujitambua, uthubutu, kufanya maamuzi sahihi na kujiwekea malengo katika maisha
yao.
Alisema programu hii inalenga katika kuboresha ustawi na
maendeleo kwa mama wadogo kwa kuwapatia fursa za uwezeshaji kiuchumi.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Tabora Baraka Makona
alisema jumla ya mama wadogo 90 kutoka mkoani humo watapata mafunzo hayo ambapo
45 wanatoka Uyui na Kaliua 45.
Alisema wameamua kuanzia Wilaya hizo kwa sababu ndizo
zinaongoza kwa mimba na ndoa za utotoni.
Mafunzo hayo yanaendeshwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa
kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora na Halmashauri za Wilaya ya Tabora
-Uyui na Kaliua.
No comments:
Post a Comment