HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 04, 2019

WATUMISHI WATANO WA UYUI MATATANI KWA KUSHINDWA KUSIMAMIA KILIMO

NA TIGANYA VINCENT, TABORA

SERIKALI ya Mkoa wa Tabora imeagiza kukamatwa kwa mkulima wa pamba wa Kitongoji cha Mlimani na kuchukuliwa hatua za kinidhamu watumishi watano wa Halmashauri ya Wilaya ya Tabora-Uyui kwa tuhuma za kuvunja Sheria na Kanuni 10 za zao la Pamba na kudhofisha kilimo cha zao la pamba katika maeneo mbalimbali  wilayani humo.

Agizo hilo limetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za kilimo wilayani humo na kukuta baadhi ya wakulima wakiwa wamevunja Sheria na Kanuni 10 cha kilimo cha zao la pamba.

Alisema mkulima wa Kitonji cha Mlimani katika Kata ya Loya Mansor anatuhumiwa kwa kosa la kukatia mabaki ya pamba ya msimu uliopita na kuifanya ichipue upya na kisha kuanza kuipalilia kwa nia ya kutaka kuivuna msimu ujao , jambo ambalo ni kosa.

Mwanri alisema kitendo hicho kinaweza kusababisha magonjwa na wadudu wa msimu uliopita kuhamia katika mazao ya msimu huu wa kilimo na kushusha uzalishaji.

Mkuu huyo wa Mkoa aliagiza watumishi hao wa Halmashauri hiyo kuchukuliwa hatua hiyo kwa sababu wameshindwa kutekeleza majukumu yao na kusababisha wakulima wavunje Sheria na wengine wasilime zao hilo kutokana na vikwazo wanavyopata kutoka kwa Kampuni mbalimbali za usambazaji mbegu katika eneo hilo.

Alisema watendaji hao ambao wanalipwa na Serikali kutokana na kodi za wakulima na wafanyabiashara wakati wanashindwa kuwahudumia ili waweze kuzalishaji kisasa na kuzingatia kanuni za kilimo bora.

Mwanri aliwataja watumishi ambao wanatakiwa kuchukuliwa hatua kuwa ni Kaimu Mkuu wa Idara ya Kilimo (DAICO), Afisa Ugani wa Kata ya Loya , Afisa Ushirika wa Uyui , Mtendaji wa Kijiji cha Kigwa Kijiji (Nzigala) na Mtendaji wa Kata ya Kigwa.

Alisema kuwa Mtumishi wa Umma ambaye anaona kuwa hawezi kwenda na kasi ya uongozi wa Awamu Tano ni vema akajiondoa taratibu ili awapishe wale ambayo wako tayari kuwatumikia wananchi.

No comments:

Post a Comment

Pages