NA TIGANYA VINCENT
VYAMA Vikuu vinavyolima zao
la Tumbaku Nchini (TCJE) vimeazimua kuanza ujenzi wa kiwanda cha
kuchakata Tumbaku mkoani Tabora .
Lengo la vyama hivyo ni kupata kiasi cha shilingi
milioni 700 hadi mwisho wa msimu wa kilimo cha tumbaku mwaka huu kwa ajili ya
ujenzi wa kiwanda hicho
Kauli hiyo imetolewa juzi mjini Tabora na Mwenyekiti
wa Umoja wa Vyama Vikuu vya Ushirika wa Wakulima wa Taumbaku hapa nchini
Emanuel Charahani wakati wa mkutano wa 26 wa Chama Kikuu cha Ushirika wa
Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU).
Alisema kuwa wazo la kiwanda hicho limeshajadiliwa
na wajumbe wa vyama vyote ikiwemo cha Kigoma, Kahama na Mpanda na kuafikiwa
sasa kilichobaki ni utekelezaji tu.
Charahani alisema wajumbe wa Mkutano
Mkuu wa WETCU kwa kauli mmoja wameazimia kujengwa kwa kiwanda cha kuchakata zao
la tumbaku wilayani Urambo mkoani Tabora.
Alisema kiwanda hicho kitasaidia sana kuhamasisha
kilimo bora cha tumbaku na kuongeza uzalishaji maradufu tofauti na hali ilivyo
sasa.
Charahani alisema hakika vyama hivyo wamedhamiria kujenga
kiwanda hicho ambacho kitaondoa urasimu wa makisio na kuongeza tija
katika uzalishaji wa Tumbaku na zaidi ya ajira 3000 zipatikana kila
msimu wa kilimo cha Tumbaku .
Alisema ili kufanikisha ujenzi huo alishauri
Wenyeviti na Mameneja wa vyama vikuu vya ushirika, Wenyeviti na Wakurugenzi wa
halmashauri zinazolima zao la tumbaku, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa na
Mrajisi wa Mkoa wakutane Aprili 15, 2019 katika Ofisi za Bodi ya Tumbaku
Tanzania ili kuunda kamati ya utekelezaji.
Charahani alishauri kuanza mara moja kwa mchakato
na upembuzi yakinifu huku akiutaka uongozi wa WETCU kusimamia ipasavyo zoezi
hilo ili kuharakisha ujenzi.
Alisema kwamba hizo ni juhudi za wakulima
kuhakikisha wanaungana wadau kuunga mkono jitihada za serikali ya
awamu ya Tano dhidi ya viwanda.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya
wilaya ya Uyui Said Ntahondi alisema kuwa ujenzi wa kiwanda hicho unasubiriwa
kwa hamu kubwa na wakulima wa tumbaku hapa nchini kutokana na umuhimu wake.
Alisema wazo la ujenzi wa kiwanda hicho limepata
baraka za vyama vyote vikuu vya ushirika wa wakulima wa zao hilo katika mikoa
yote na kila mkulima amekubali kuchangia sh 9 kwa kila kilo atakazouza ili
kufanikisha ujenzi huo.
Ntahondi alisema kwa kuchangia kiasi hicho katika
msimu huu pekee wanatarajia kukusanya zaidi ya sh milioni 700 kwa ajili
ya kazi hiyo ambapo kinatarajiwa kujengwa kule Urambo ndani ya mkoa huo na eneo
tayari limeshapatikana.
Alisisitiza kuwa kiwanda hicho ni mwarobaini wa
kero ya muda mrefu ya mkulima kuwekewa ukomo wa kilo za kuzalisha wakati ana
uwezo wa kuzalisha zaidi ya kiwango hicho.
Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini Collins
Nyakunga aliutaka uongozi wa Halmashahuri ya wilaya ya Urambo kukaa meza moja
na Vyama Vikuu vya Ushirika vya Milambo na WETCU kabla ya kuanza ujenzi huo ili
kuepusha migongano ya ardhi.
No comments:
Post a Comment