Mbunge wa Viti Maalum anayewakilisha vijana, Zainabu Katimba, akizungumza na baadhi ya vijana wanaowakilisha makundi mbalimbali jijini Dar es Salaam wakati wa kongamano aliloandaa lenye dhamira ya kuangalia fursa za kiuchumi zinazoweza kufanywa na vijana kwa ajili ya kukuza uchumi wao. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Friedrich Ebert Stiftung (FES), Andreas Quasten, ambayo imeshirikiana na mbunge kuwezesha kongamano hilo. (Na Mpiga Picha Wetu).
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
VIJANA
mbalimbali nchini Tanzania, wameaswa kuchangamkia fursa mbalimbali za
kiuchumi, ikiwamo namna bora ya kuungana vikundi ili kuomba fedha za
Halmashauri ambazo zimekuwa zikikosa waombaji katika maeneo mengi, huku
sababu kubwa ni uelewa mdogo juu ya upatikani wa fedha hizo zinazotolewa
maalum ili kuwakomboa vijana kiuchumi.
Hayo
yamesemwa na Mbunge wa Viti Maalum, akiwakilisha vijana katika Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Zainabu Katimba, katika kongamano la
vijana aliloandaa kwa kushirikiana na taasisi yake ya WEZESHA,
akishirikiana pia na Taasisi ya Friedrich Ebert Stiftung, ikikutanisha
viongozi wa makundi mbalimbali jijini Dar es Salaam, nchini hapa.
Akizumgumzia
changamoto hizo, mheshimiwa Katimba alisema kuwa wapo watu wanaoamini
kuwa fedha hizo hazipo au zinatoka kwa watu maalum, bila kujua kwamba
fedha hazitoki kwa watu mmoja mmoja na kinachotakiwa ni kuungana katika
makundi na kuanisha vipengele vya kimkakati, jambo ambalo limekuwa
halifanyiki.
"Mimi nawakilisha vijana kule
bungeni, lakini pia tunaelekea kwenye bajeti mpya, hivyo naamini pamoja
na mambo mengine, tukitoka kwenye kongamano hili la kuwezesha a,
kuelimishana sambamba na kufungua milango ya kuiona fursa, naamini
tutakuwa katika nafasi nzuri, zaidi uwezo wa vijana kuzichangamkia pia
fedha za serikali katika Halmashauri zetu.
"Nimekuwa
nikifanya makongamano haya kwa muda mrefu na dhamira yetu kubwa ni sisi
vijana wenyewe kujitambua, kwa sababu tunapoweza kutumia fursa
tunazokutana nazo mtaani, walau tunaweza kujikwamua kiuchumi na
kulikomboa pia Taifa letu ambalo sera ya viwanda imeshika kasi na sisi
vijana wenyewe ndio nguvu kazi ya Taifa kwa namna moja ama
nyingine,"Alisema Katimba, ambaye pia ni mwasisi wa taasisi ya Wezesha.
Akizumgumzia
kongamano hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Friedrich Ebert Stiftung
(FES), Andreas Quasten, alimpongeza Mbunge wa Viti Maalum, Zainabu,
kwakuwa karibu na vijana akisema anawawakilisha vizuri bungeni.
"FES
tunampongeza bi Zainabu kwa kufanya mambo mengi yanayohusu vijana,
ambapo tunaamini kwa uwapo wake bungeni, unasaidia kuwezesha vijana,
katika kipindi hiki ambacho idadi kubwa ya watu Tanzania ni vijana, huku
wakiwa na changamoto nyingi ikiwamo ajira, ushiriki katika mambo ya
kijamii, kisiasa na kiuchumi.
"Sisi FES
tutaendelea kushirikiana na makundi yote sambamba na serikali Kuu ili
kuhakikisha kwamba changamoto hizo zinakwisha ili kuwafanya vijana na
Watanzania wote wanaishi maisha vizuri, sanjari na uelewa mpana wa
kutumia fursa endelevu za kiuchumi,"Alisema.
Katika
kongamano hilo la siku moja lililofanyika katika ofisi Kuu za FES
zilizopo Kinondoni, Morocco, jijini Dar es Salaam, vijana mbalimbali
walichambua changamoto wanazokutana nazo mitaani, bila kusahau mwelekeo
unaoatakiwa kufuatwa katika Bajeti Kuu ya Serikali itakayosomwa baadaye
mwaka huu bungeni, jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment