HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 14, 2019

SERIKALI, KAMPUNI YA TOTAL KUTAFITI MAFUTA TANZANIA

Makamu wa Rais wa Kampuni ya Mafuta ya Total Kanda ya Afrika, Kaskazini, Kati na Afrika Mashariki, Jean Philippe Torres (wa kwanza kulia), Rais wa Total Africa, Stanislas Mittelman (wa pili kulia), Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Total Tanzania,Tarik Moufaddal (wa tatu kulia), wakibadilishana mawazo na Mariane Saw, (wa kwanza kushoto), na Marsha Msuya Kileo, Mwanasheria na Mkurugenzi wa Uhusiano wa Total, wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya Total Tanzania, jijini Dar es Salaam juzi. (Na Mpiga Picha Wetu).


NA SALUM MKANDEMBA


SERIKALI ya Tanzania kwa kushirikiana na Kampuni ya Mafuta ya Total, itafanya utafiti wa mafuta nchini, ambayo yakipatikana yataubadili uchumi wa Tanzania kwa kuongeza kasi ya kuifanya nchi ya Uchumi wa Kati, kutegemeana na kiwango cha mafuta kitakachogunduliwa.


Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nishati, Medard Kalemani, wakati wa hafla ya kuwapongeza wafanyakazi na wadau wa Total Tanzania, katika Maadhimisho Total Kutimiza Miaka 50 nchini Tanzania, yanayoadhimishwa kwa wiki nzima kwa shughuli mbalimbali.

Sherehe ya Jubilee ya Maadhimisho hayo imefanyika katika Hotel ya Hyatt Regency, Kilimanjaro, jijini Dar es Salaam, ambako imeelezwa kuwa kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania itakuwa kubwa, utakaoibadili kabisa taswira ya Tanzania kiuchumi.


Waziri Kalemani alisema utafiti umethibitisha kuwa, kila mahali ilipogunduliwa gesi asili chini yake kuna mafuta, hivyo Serikali imeanza mazungumzo na Kampuni ya Total Tanzania, ili kufanya utafiti wa mafuta, hivyo kuwataka Watanzania kuipatia kila aina ya ushirikiano kampuni hiyo mshirika muhimu wa maendeleo.


Aliipongeza Kampuni ya Total kwa kazi zake kubwa sita zinazozifanya nchini Tanzania, ikiongozwa na kuuza mafuta yanayoongoza kwa ubora, vilanishi vyenye ubora wa hali ya juu, ikiwa ni pamoja na kujenga bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanga Tanzania.


Pia, Waziri Kalemani alibainisha kuwa Total inasambaza nishati mbadala ya nishati jua, inatoa ajira za kudumu na za muda kwa Watanzania wengi, na kubwa zaidi ni kwa Total kuchangia huduma kwa jamii, yote hayo ukiyajumlisha, yanachangia maendeleo ya taifa.


Kwa upande wake, Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Total Tanzania, Bw. Tarik Moufaddal, alisema katika kipindi cha miaka 50, Kapuni ya Total imefanya makubwa Tanzania, kufikia kuwa ndio kampuni inayoongoza kwa wingi wa vituo vya kuuza mafuta yanayoongoza kwa ubora na na vilanishi vyenye ubora.


Sherehe za Maadhimisho hayo, zilizinduliwa wiki iliyopita na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, ambapo pamoja na mambo mengine, aliwakabidhi zawadi mbalimbali wafanyakazi wa muda mrefu wa Total Tanzania na wadau wa kampuni hiyo. 



Total Tanzania ni kampuni ya mafuta ya petroli ambayo iliingia Tanzania mwaka1969, ambako hadi sasa inatumia utaalamu wake katika kutoa huduma za kuaminika kwa wateja wake kwa mfumo wa kadi maalum ‘Kadi ya Total’ kwa ajili ya ununuzi wa mafuta na huduma mbalimbali magari katika vituo vya mafuta vya Total.


Kwa mujibu wa Moufaddal, hayo yote yanafanyika katika kujitanua kibiashara kuelekea kwenye matumizi ya nishati mbadala,na kwamba Total Tanzania kupitia mradi wake wa Total Access to Solar (TATS Project), inasambaza taa za nishati jua zinazoitwa AWANGO kwa jamii ya Watanzania.

No comments:

Post a Comment

Pages