Na Peter Haule, Farida Ramadhani-WFM, Dodoma
Serikali imesema kuwa Vituo
vyote vya huduma ndani ya Ofisi za Shirika la Posta vimeunganishwa kwenye
mtandao na mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano- TEHAMA wa Benki ya
TPB kwa wateja wa vijijini na pembezoni
mwa miji, ili kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa wakati kama ilivyo kwa
wateja wengine wanaohudumiwa na matawi makubwa na madogo
Hayo yameelezwa Bungeni
jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb)
alipokuwa akijibu swali la Msingi la Mbunge wa wa Tumbatu Mhe. Juma Othman Hija,
aliyetaka kujua iwapo Benki ya TPB imefikia malengo ya kupeleka huduma vijijini
na maeneo yasiyofikika kwa urahisi.
Dkt. Kijaji alisema kuwa lengo
la Benki ya TPB ni kuongeza wigo wa
biashara ya benki kwa kutumia teknolojia ya kisasa katika maeneo ya vijijini,
hivyo Benki hiyo imefanikiwa kuboresha huduma katika ofisi 200 za Shirika la
Posta Tanzania kwa kutumia teknolojia ya TEHAMA inayomuwezesha mwananchi kupata
huduma za kibenki kupitia simu za kiganjani, mawakala wa kampuni za simu pamoja
na mashine za kutolea fedha (ATM) .
“Benki ya TPB imeongeza idadi ya matawi makubwa kutoka 30
kwa mwaka 2017 hadi 36 kwa mwaka 2018 na matawi madogo yaliongezeka kutoka 37 mwaka 2017 hadi kufikia 40 kwa
mwaka 2018, yakiwa yanawawezesha wateja kupata huduma bila kutembelea matawi
walipofungulia akaunti zao”, alieleza Dkt. Kijaji.
Alisema kuwa Idadi hiyo ya
matawi inahusisha matawi yaliyokuwa ya Benki ya Twiga na Benki ya Wanawake
Tanzania, aidha jumla ya akaunti 227,052 zilifunguliwa na wananchi wa vijijini
na pembezoni mwa miji kwa kutumia mfumo wa kibenki kwa njia ya simu za
kiganjani unaojulikana kama TPB Popote.


No comments:
Post a Comment