June 13, 2019

Bandari ya Dar es Salaam yakamilisha ujenzi wa ghati namba moja

Na Janeth Jovin

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,  Isack Kamwele (pichani), amesema kuwa kukamilika kwa ghati namba moja yenye urefu wa mita 191 katika Bandari ya Dar es Salaam itaweza kupokea meli kubwa zenye uwezo wa kubeba kontena 4000 hadi 7000.

Waziri Kamwele ameyasema hayo jijini Dar es Salaam katika bandari hiyo wakati wa hafla fupi ya kukabidhi gati hiyo ambayo ipo katika utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa bandari ya Dar es Salaam ambapo kwa awamu ya kwanza zaidi ya Bilioni 300 zimeshatumika. 

Kamwelwe amesema kabla ya ghati hiyo kuwepo, walikuwa wakipokea kontena 2, 000 hadi 2,800, hivyo  baada ya kuanza kazi kwa ghati hiyo itakuwa na uwezo  wa kupokea meli zenye kontena za mizigo kati ya 4,000 hadi 7,000.

"Katika Bandari hii ya Dar es Salaam Rais alisema atatafuta fedha ili iweze kuboreshwa na tayari fedha zimepatikana na kazi ya kuiboresha imeshaanza hivyo niwaombe watendaji na wakandarasi wajitahidi kukamilisha haya mambo mapema ili tuweze kupokea mizigo mingi ya wafanyabiashara itakayokuwa inaiingizia Serikali mapato, " alisema 

Alisema upanuzi wa ghati namba moja hadi nane  utasaidia bandari hiyo kuhudumia tani milioni 25 kutoka milioni 16.2 inayohudumia sasa

Kwa mujibu wa TPA, ghati hiyo iliyokamilika  ni sehemu ya ghati nane zitakazojengwa kwa Sh.Bilioni 968 fedha za mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Uingereza.

No comments:

Post a Comment

Pages