June 12, 2019

BIBI ATOKWA NA MACHOZI AKIISHUKURU HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI-MLOGANZILA

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Daktari Julieth Magandi, akimuinua Patricia Hilary ambaye ni bibi wa mtoto Hilary Pllasdius (8) aliyepiga magodi kushuru kwa msaada wa kiti cha kutembea pamoja na kusamehewa gharama za matibabu.


Na Asha Mwakyonde
 
MWANAFUNZI wa Shule ya Awali ya Millennium iliyopo Kijichi jijini Dar es Salaam, Hilary Pllasdius (8), amekaa miezi minne katika Chumba Maalum cha Uangalizi (ICU) huku akipumulia mashine kwa miezi mitatu baada ya kuugua ugonjwa wa kupooza mwili.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo wakati wa kuruhusiwa mtoto huyo, Daktari Bingwa wa Watoto, Mwanaidi Amiri, amesema kuwa alifikishwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili - Mloganzila kuanzia Oktoba mwaka jana na kuendelea kupatiwa matibabu.

Daktari huyo amesema kuwa Hilary alifikishwa hospitalini hapo akiwa na shida ya kupooza kwa mwili kuanzia miguuni hadi kwenye shingo na kumsababishia kupumua kwa shida na kwamba ugonjwa huo unaitokea kwa watu wazima na watoto.
"Ugonjwa huo mara nyingi unatokea baada ya mtu kupataka maambukizi ya bakteria kupitia mfumo wa kifua au mtoto akiharisha,mwili wake ukiwa unashambulia mishipa ya fahamu na kusababisha mishipa yake kukosa nguvu na kujikuta anashindwa kunyanyua miguu ,”anasema daktari Mwanaidi.

Anasema baada ya Hilary kupata ugonjwa huo ulienda kwa haraka sana ambapo siku waliyompokea alijikuta anashindwa kupumua.

Daktari Mwanaidi anaongeza kuwa kwa sababu ya kushindwa kupumua walimpeleka ICU kutokana na mishipa yake kuwa dhaifu ambapo alikaa miezi minne na hadi sasa ana miezi nane hospitalini hapo.

“Kwa sasa amepata nafuu na anaweza kunyanyua miguu na mikono hali ambayo tumeamua kumruhusu arudi nyumbani na kuendelea na mambo mengine ikiwamo kwenda shule,”anasema.

Naye Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Daktari . Julieth Magandi, amesema wanafuraha kwa mtoto huyo kuruhusiwa kwani alikuwa ICU muda mrefu.

Mkurugenzi huyo anaeleza kuwa gharama za mtoto huyo zilizotumika ni zaidi ya Sh milioni 17 katika matibabu yake.
“Bibi yake hakuweza kulipa hizi gharama sisi tumeangalia kumtibu kwanza na Hospitali imetoa msamaha wa gharama za matibabu. Matibabu yake ni makubwa kwa upande wa dawa dozi moja ni Sh 700,000 kwa siku utaona matibabu ya ICU yana gharama kubwa,” amesema.

Amesema hospitali hiyo imempatia msaada wa kiti mwendo kwa ajili ya kumsaidia kutembelea chenye gharama ya Sh. 450,000.

Kwa upande wake Bibi wa mtoto huyo, Patricia Hilary, ameushukuru uongozi wa hospitali hiyo pamoja na wafanyakazi wake kwa msaada mkubwa waliompatia kwani madaktari walijitahidi kupambana na afya ya mtoto huyo na hatimaye leo wameruhusiwa.

Patricia anaeleza kuwa katika kumuuguza mjukuu wake baadhi ya watu walimkatisha tamaa kwa madai kuwa mtoto huyo hawezi kupona jambo ambalo madaktari wamemsaidia na kumponya.

Hata hivi Patricia amejikuta anatokwa na machozi baada ya kusikia amesamehewa deni lake pamoja na kupatiwa msaada wa kiti cha kutembelea mtoto huyo.

No comments:

Post a Comment

Pages