June 12, 2019

Askofu Pengo: Waamini wa Kanisa Katoliki wanamchango mkubwa katika kulifanya kuwa na uhai

Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycap Kardinal Pengo, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Halmashauri ya walei Tanzania.

Na Janeth Jovin

ASKOFU Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam Mwadhama Polycap Kardinal Pengo amesema kuwa waamini wa kanisani katoliki wanamchango mkubwa katika kulifanya kanisa hilo kuwa na  uhai na maendeleo kwa ujumla. 

Kardinal Pengo ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya Halmashauri ya walei Tanzania yanayotarajiwa kufanyika Juni 16 mwaka huu viwanja ya Msimbazi Center jijini Dar es Salaam. 

Alisema licha ya michango mbalimbali ikiwamo zaka inayotolewa na waamini wa kanisa hilo pia ndio watu pekee wanaosababisha kanisa hilo kuwa na uhai hadi leo. 

"Katika kutambua mchango huo,  Juni 16 katika viwanja vya Msimbazi Center tutaadhimisha Jubilei ya miaka 50 ya halmashauri ya Walei Tanzania watu ambao wamekuwa wakiwaongoza vema waamini wetu katika kufanya mambo mbalimbali yanayohusu Kanisani na jamii. 

Hatua waliopiga ya kuwafanya waamini watoe michango yao, kukaa kwa pamoja na kuelewana tena kwa kufanya kazi kwa weledi hakika ni kubwa mno, tunawashukuru na kumshukuru Mungu kwa hilo, " alisema. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Taifa, Gasper Makiluli alisema maadhimisho ya Jubilei hiyo yanawapa nguvu ya kuendelea kufanyakazi kwa bidii na kwa kushirikiana. 

Mkuu wa Idara ya Walei Baraza la Maaskofu Tanzania Padri Raphael Madinga alisema uwepo wa Jumuiya ndogo ndogo ni moja ya mafanikio yanayodhirisha kazi zinazofanywa  utume huo wa walei hapa nchini. 

Naye Katibu Msaidizi wa halmashauri hiyo, Donesta Byanigaba alisema maadhimisho ya Jubilei hiyo yataanza kwa maandamano Juni 16 mwaka huu katika Kanisa la St Joseph,  Magomeni na Buguruni kuelekea Msimbazi Center mahali ambapo ibada ya misa takatifu itakapoadhimishwa.

No comments:

Post a Comment

Pages