June 10, 2019

Hospitali ya Aga Khan kufanya upasuaji bure kwa wanawake na watoto walioungua na moto

Na Janeth Jovin

HOSPITALI ya Aga Khan kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (NMH)  na madaktari bigwa kutoka nchini Marekani wanatarajia kuwafanya upasuaji bure kwa wanawake na watoto wa kike waliopata majanga ya kuungua moto, ajali na kufanyiwa ukatili wa kijinsia.

Zaidi ya watu 100 kutoka mikoa mbalimbali nchini  wanatarajia kuwafanyia upasuaji huo, ambapo zoezi hilo litakuwa na awamu mbili na awamu ya kwanza itaanza rasmi Juni 15 mwaka huu kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 8:mchana katika hospitali ya Aga Khan.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Jana,  Daktari Bingwa wa upasuaji kutoka Hospitali ya Aga Khan,  Dk. Aidan  Njau alisema  upasuaji huo utafanywa bure katika hospitali hiyo ya Aga Khan  na wanatarajia  wagonjwa 100 watapatiwa matibabu hayo.

Alisema anatambua kuwa upasuaji huo ni gharama kubwa lakini wao kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wataendesha zoezi hilo bila malipo kwa kinamama na watoto wa kike watakaojitokeza na kugundulika kuwa na matatizo hayo kwa kiwango kikubwa.

"Zoezi hili tumelianza tangu mwaka 2016 na kiukweli limewanufaisha kinamama wengi hata hivyo tumekuwa tukilifanya mara moja kwa mwaka ila mwaka huu tutalifanya mara mbili na watu 100 tunatarajia kunufaika.

Ushirikiano huu uliyopo baina ya hospitali hizi mbili na wenzetu kutoka nje ni mzuri kwani unatatusaidia kuweza kubadilisha ujuzi, wagonjwa kutibiwa bure hivyo tunawaomba watanzania wenzetu wenye majanga hayo wasisite kujitokeza kwa lengo la kupata huduma, " alisema.

Alisema katika zoezi hilo pia watawatibia wakimama wanaosumbuliwa na saratani ya shingo ya kizazi pamoja na ya matiti ambayo ameeleza kuwa zimekuwa zikisababisha vifo vingi nchini.

"Tutafanya oparesheni ya kutengeneza ziwa kupitia kwenye nyama za mwanamke aliyepata saratani ya ziwa, tunaamini mwanamke aliyekatwa ziwa akifanyiwa oparesheni hiyo na kupata ziwa lingine  tutamuongezea uwezo wa yeye kujiamini na kupunguza kunyanyapaliwa, " alisema.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji Hospitali ya Aga Khan Dk. Athar Ali alisema wagonjwa wamekuwa wakiongezeka kila mwaka hivyo kwa mwaka huu watafanya zoezi hilo mara mbili ambapo awamu ya kwanza watawahudumia wagonjwa 40 hadi 50 na awamu ya pili watu 50.

"Gharama ya matibabu haya kwa mgonjwa mmoja ni zaidi ya Milioni tano ila sisi tufanya bure hivyo tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi pindi tunapotangaza kufanyika kwa upasuaji huo wanawake wote wenye majeraha hayo ya kuungua, " alisema.

Kwa upande wake Mwazilishi wa Taasisi isiyokuwa ya Kiserikali inayojishughulisha na masuala ya kijamii ya Sadaka, Dk. Ibrahim Msengi alisema wao waliguswa na matatizo hayo yanayowakumba wanawake hivyo wakaamua kushirikiana na hospitali hizo pamoja na kukusanya fedha kwa wadau mbalimbali kwa lengo la kufanikisha zoezi hilo.

No comments:

Post a Comment

Pages