June 13, 2019

JESHI LA POLISI LAWAMANI IRINGA

Meneja wa Bar ya Shine Pub ya mkoani Iringa, Richard Sanga, akitoa kero yake mbele ya wanahabari. (Picha na Denis Mlowe).

Mmoja wa wamiliki wa bar akizungumza mbele ya mkuu wa wilaya walipofika ofisini kwake kuzungumza juu ya malalamiko ya jeshi la polisi.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela akizungumza na wamiliki wa bar na mameneja mara baada ya kuwasikiliza malalamiko yao ya kufanyiwa vurugu na polisi nyakati za usiku.


 
Na Denis Mlowe, Iringa

WAMILIKI wa bar na klabu za usiku mkoani Iringa wamepinga na kulalamikia kitendo cha jeshi la polisi mkoani Iringa kuwafanyia vitendo vya kupiga wateja na wahudumu kwa kile kinachosemekana muda wa kufunga bar kuzidishwa.

Wakizungumza mara baada ya kuandamana hadi kwa Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela, wafanyabiashara hao Zaidi ya 30 wanaomiliki bar mkoani hapa walisema kuwa kitendo kinachofanywa na baadhi ya askari wa jeshi hilo wanaofanya doria nyakati za usiku wamekuwa wakiwapiga wateja na wahudumu pindi wakikuta muda wa kufunga bado ni kitendo kinachohatarisha Amani.

Mmoja wa wamiliki wa Bar mkoani hapa  aliyezungumzia hali hiyo, Happy  Matanji alisema kuwa tarehe 8 mwezi huu walipita polisi katika bar anayomiliki wakaamuru bar ifungwe lakini walitumia nguvu kubwa  na kuanza kuwapiga wateja na wahudumu na kila mtu aliyeonekana katika eneo hilo licha ya kuwa na kibali kinachoruhusu kutoa huduma muda wa zaida.

Alisema kuwa manispaa walimpatia kibari ambacho nikaruhusu kufunga bar hiyo hadi saa nane badala ya muda wa saa sita lakini askari waliokuwa doria hawakutaka kabisa kusikiliza  wala kukubaliana na kibari ambacho kinaruhusu kufungwa kwa huduma za bar kutokana na kibari hicho.

Alisema kuwa meneja wa bar hiyo alichukua jukumu la kwenda kituo cha polisi kupata msaada Zaidi lakini alipofika kituoni walimweka ndani kwa kumwambia kwamba hadi kituoni amewafata licha ya kuwa kibali cha kufanya biashara hadi muda huo.

“Unaamua kuepusha shari na kufata sharia ya kuomba kibali lakini cha kushangaza mamlaka ya jeshi la polisi wanakuwa hawakitambui na mwisho wa siku wateja na wahudumu wanaambulia kipigo hapo unakuwa unaingia hasara kubwa ya kulipia kibali na hela kupotea na haitoshi wanapelekwa mahabusu sasa hapo inakuwaje” alisema

Alisema kuwa alichukua jukumu la kumpigia kamanda wa jeshi la Polisi mkoa wa Iringa na kumwabarisha kuhusu hali hali na kusema kuwa analifanyia kazi na kumjulisha laki alipotafutwa siku ya pili hakuweza kupokea simu na juzi alipopigiwa rpc alisema kuwa yuko katika kikao atapigiwa lakini hakuna hatua yoyote ile.

Matanji aliongeza kuwa anashangaa kwa kiasi kikubwa ni mafunzo ya aina gani wanayopatiwa jeshi la polisi kutumia nguvu kubwa katika kuwakabili wateja ambao hawana shida yoyote hali ambayo inawashangaza wengi kwani hapo awali hali hii haikuwepo.

Richard Sanga meneja wa bar ya Shine Pub alisema kuwa vitendo ambavyo wanafanya jeshi la polisi limefanyika katika bar hiyo na kusema kwamba leseni za biashara hazionyeshi ni muda gani wa biashara hiyo inafungwa saa ngapi tofauti na leseni za zamani zilizokuwa zinaonyesha muda wa kufungua na kufunga hivyo unaambiwa tu unatakiwa kufunga muda Fulani.

Alisema kuwa polisi anapofanya kazi yake inabidi afate uongozi wa eneo husika na kufanya mazungumzo kwamba muda wa kufunga umewadia ikiwezekana kumshauri na kumpa onyo ila wao wakifika hakuna onyo wala ushauri wowote kikubwa ni nguvu mwanzo mwisho na kutoa amri za watu kukaa chini licha yaw engine kuwa wamekaa hapo ndipo hasara inaanza kwani wengi wa wateja wanakuwa wanadaiwa bili lakini nguvu inayotumika ni kubwa.

Alisema kuwa askari wanatembea na viboko, nyaya za umeme za kumpigia mtu bila kufikiria kwamba raia ni askari jamii na wanafanya kazi kwa Amani iweje wao watumie nguvu badala ya kujenga ushirikiano ambao utasaidia kuwabaini wahalifu na kuuweka mji kuwa sawa lakini askari wa doria wakija wao na mabavu kwa kila mtu ndani ya bar na kisha wanakamatwa na kupelekwa mahabusu.


Alisema kuwa faini inayotolewa mahakamani ni kubwa Zaidi kuliko ilivyowekwa kisheria ambapo unakuta mtu unalipa Zaidi ya laki sita kwa kuwalipia faini wahudumu sita wa bar waliofikishwa mahakamani hapo na mbaya Zaidi wanakuwa hawana makosa kwa kuwa wanakuwa wanakamatwa katika eneo la kazi lakini wanafunguliwa makosa uzembe na uzururaji.

Sanga aliongeza kuwa biashara wanayofanya wanakumbuna na changamoto nyingi sana ambazo nyingine wanashindwa kukabiliana nazo zikiwemo utitiri wa kodi lakini licha ya hivyo muda wa kufanya biashara mchache na hapo unakutana na changamoto nyingine ya doria na wateja kuondoka na bili.

Akiwajibu wamiliki wa bar waliofika ofisini kwake, Mkuu wa wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alisema kuwa mzunguko wa fedha kwa asilimia kubwa unaletwa na wamiliki wa sehemu za vinywaji na kukiri kuwa jeshi la polisi limefanya kosa na kuwaomba msamaha kwa wamiliki wa bar na klabu kwa niaba ya jeshi la polisi.

Kasesela ambaye na Mwenyekiti wa Usalama wa Wilaya ya Iringa alisema kuwa awali hakukuwa na tabia kama hiyo hivyo ataongea na kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Iringa na kubaini nini hasa chanzo ambacho kinasababisha haya yote ambayo yanatokea sasa kwa wahudumu na wateja wa bar.

Alisema kuwa kwa upande wa jeshi la polisi na serikali walitalifanyia kazi na kuwahakikishia kuwa hakuna askari atakayepona endapo atabainika kuwanyanyasa Watanzania wenzake bila sababu na kutangaza kwa wamilki wa bar na pub zote wilaya ya Iringa mwisho wa kufunga ni saa sita na ikifika saa tano wamiliki wa bar wanatakiwa kupunguza sauti ya muziki na ikifika muda was aa saba askari wasiwabugudhi wateja.

No comments:

Post a Comment

Pages