June 13, 2019

TAIFA STARS KUZINDUA JEZI MPYA ZA AFCON 2019 LEO IKIJIPIMA KWA MISRI 'THE PHARAOHS'

 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati ya Ushindi ya Taifa Stars, Paul Makonda, akizindua jezi itakayotumiwa na Taifa Stars katika AFCON 2019.
 Taifa Stars iliyoichapa Uganda na kufuzu AFCON 2019.


Alexandria, Misri

KATIKA kujiandaa na Fainali za Mataifa Afrika (AFCON 2019), kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars,’ leo saa 4:00 usiku (kwa saaa za Afrika Mashariki), kinashuka dimbani mjini Alexandria, nchini Misri kuumana na wenyeji wao, kwenye Uwanja wa Bourg Al Arab.

Taifa Stars, inayodhaminiwa na Bia ya Serengeti, inayozalishwa na Kampuni ya Serengeti Breweries (SBL), ikiwa chini ya Kocha Mkuu, Mnigeria Emmanuel Amunike, inajiandaa kucheza fainali za pili za AFCON katika historia ya soka la Tanzania, baada ya kufanya hivyo mwaka 1980.

Katika fainali za AFCON 2019, Tanzania imepangwa Kundi C, pamoja na mataifa Algeria, Senegal na Kenya. Kikosi hicho ambacho leo kinazindua jezi mpya, kitaanza mechi zake tatu za Kundi C, dhidi ya Senegal Juni 23, kisha kuivaa Kenya Juni 27 na kumaliza na Algeria Julai 1.

Kikosi cha wachezaji 23 wanaoendelea na mazoezi kujiandaa na fainali hizo ni Aishi Manula, Metacha Mnata, Aron Kalambo, Hassan Kessy, Gadiel Michael, Ally Sonso, Vicent Phillipo, Mohammed Hussein ‘Tshabalala,’ Agrey Moris, Kelvin Yondani, Erasto Nyoni na Feisal Salum ‘Fei Toto.’

Nyota wengine wa Taifa Stars ni pamoja na Mudathir Yahaya, Yahya Zayd, Frank Domayo, Saimon Msuva, Rashid Mandawa, Mbwana Samatta (nahodha), Thomas Ulimwengu, John Bocco, Farid Mussa, Adi Yusuph na Himid Mao ‘Ninja.’ 

Fainali za AFCON 2019 zitaanza kuunguruma Ijumaa ya Juni 21, ambako wenyeji Misri wataumana na Zimbabwe, katika pambano la kundi A la michuano hiyo, ambayo kwa mara ya kwanza inashirikisha mataifa 24 badala ya 16 yaliyokuwa yakishiriki katika fainali zilizotangulia. 

MAKUNDI AFCON 2019
Kundi A: Misri, Zimbabwe, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Kundi B: Burundi, Madagascar, Guinea na Nigeria
Kundi C: Tanzania, Kenya, Senegal na Algeria
Kundi D: Namibia, Afrika Kusini, Ivory Coast na Morocco
Kundi E: Angola, Mauritania, Mali na Tunisia
Kundi F: Guinea Bessau, Benin, Ghana na mabingwa watetezi, Cameroon.

No comments:

Post a Comment

Pages