June 17, 2019

NEMC yatambua michango ya wadau katazo la mifuko ya plastiki

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEM), limeshukuru taasisi na mamlaka zote ambazo zimesimama imara na kufanikisha zoezi la kuondoa mifuko ya plastiki nchini.

Akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Samuel Gwamaka (pichani), ameishukuru kipekee Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kutoka ngazi ya kata mpaka taifa na kueleza kazi ya wizari hiyo imezaa usumamizi mzuri na umekuwepo utekelezaji mzuri wa katazo hilo pasipo kuliletea taifa fedheha.

“Tunazishukuru taasisi zote na kwa kipekee kabisa ni wenzetu wa TAMISEMI kwa namna walivyolipokea katazo hili, wakalibeba na kulisimamia kikamilifu katika maeneo yao kuanzia ngazi za chini za kiuongozi mpaka taifa,” alisema Bwana Gwamaka.


Dk. Gwamaka amesema kuwa, licha ya mafanikio hayo bado zipo changamoto chache na kutaja moja kuwa ni kwamba kuna viwanda vinavyozalisha mifuko batili. Ameomba ushirikiano kutoka kwa wadau, hasa TAMISEMI, katika kusaka viwanda hivyo ili wamiliki wachukuliwe hatua za kisheria.

Zoezi la kusaka wamiliki wa viwanda hivyo limeanza jijini Dar es Salaam Alhamisi wiki hii.

Aidha Mkurugenzi huyo amesema kuwa mazingira ni suala mtambuka hivyo ni vyema kila mtu akashiriki kwa namna moja au nyingine katika kufanikisha utekelezaji wa katazo hilo ili kuyafanya mazingira Tanzania yawe rafiki kwa kizazi cha leo na kesho

“Mazingira ni suala muhimu kwa kila mtanzania, hivyo tunalojukumu la kuhakikisha watu wote wanaohujumu zoezi hili wanabainishwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria kwani viwanda bubu vipo huko mitaani ambako jamii kubwa inaishi,” alisistiza Dkt Gwamaka

“Zoezi hili la kuvibaini viwanda vinavyoendelea kuzalisha mifuko ya plastiki linaweza kufanikiwa sana iwapo viongozi wa serikali za mitaa, kata, wilaya na mikoa watashirikiana vyema na maofisa wa NEMC ambao watakuwa wanapita huko mitaani,” alisema Dkt Gwamaka na kuongeza

NEMC imefanikiwa kwa kiwango kikubwa katika zoezi la upigaji marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki hapa nchini kutokana na kuwepo wa vikosi kazi ambavyo vipo nchi nzima pamoja na ushirikiano baina ya viongozi wa serikali kuanzia ngazi ya mtaa mpaka Taifa.

No comments:

Post a Comment

Pages