June 13, 2019

NMB yatoa misaada S/M Liwiti, Kituo cha Afya Gairo


Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Angelina Kwingwa, akipokea madawati na vifaa vya afya kwa naiba ya shule ya msingi ya Vumila kutoka kwa Meneja wa NMB kanda ya Magharibi,Sospeter Magesse. Benki ya NMB izipiga tafu shule na vituo vya afya kwa wiki hii ikiunga mkono jitihada za Serikali kuboresha Sekta za Elimu na Afya.




Na Mwandishi Wetu

KATIKA kuunga mkono jitihada za Serikali kuboresha Sekta za Elimu na Afya, Benki ya NMB imekabidhi mabati 180 kwa Shule ya Msingi Liwiti, iliyoko Tabata, Dar es Salaam, huku ikitoa msaada wa vifaa katika Kituo cha Afya Gairo, mkoani Morogoro vyote vikiwa na thamani ya Sh. Mil. 20.

Hafla za makabidhiano hayo zimefanyika kwa nyakati tofauti jana, ambako Shule ya Msingi Liwiti imekabidhiwa mabati ya kuezekea madarasa matatu, yakiwa na tahamni ya Sh. Mil. 5, wakati Kituo cha Afya Gairo kikipokea mashuka 62, vitanda vya kulala wagonjwa vitano na magodoro yake. Pia benki hiyo wilayani Urambo imekabidhi Kituo cha afya cha Uyoga vifaa vyenye thamani ya millioni tano pamoja na madawati kwa ajili shule ya msingi ya Vumila.

Wakati msaada wa mabati kwa Shule ya Liwiti ukipokelewa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Jumanne Shauri, katika hafla iliyofanyika Liwiti shuleni, msaada mashuka, vitanda na magodoro vyenye thamani ya Sh. Mil. 5 kwa Kituo cha Afya Gairo, vilipokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Seriel Mchemba.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi mabati Liwiti Shuleni, Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Badru Idd, alisema misaada wanayotoa katika Sekta za Elimu, Afya na Majanga, inaongeza chachu ya benki hiyo kujiweka karibu na jamii, na kubaki kuwa kinara miongoni mwa taasisi zinazosapoti Serikali.

Badru aliongeza ya kwanza, misaada yao inatokana na utaratibu wa benki hiyo kupitia Kitengo cha Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kutoa asilimia moja ya faida yao ya mwaka baada ya kodi na kwamba mwaka huu wametenga kiasi cha Sh. Bilioni 1, ambako hadi sasa wametoa misaada inaayofikia Sh. Mil. 500.

Kwa upande wake, Shauri aliishukuru NMB kwa namna inavyosaidia utatuzi wa changamoto za elimu na afya wilayani Ilala, huku akisema misaada ya hiyo katika mashule wilayani humo, imesaidia kukuza kiwango cha ufaulu, ambako mwaka uliopita ilikuwa ya nne kati ya wilaya 185, ikifaulisha wanafunzzi 21,000.

Alibainisha ya kwamba, kupita misaada ya wadau muhimu kama NMB na ruzuku ya Mpango wa Elimu Bure wa Serikali ya Awamu ya Tano – unaowaingizia kiasi cha Sh. Mil. 70 kwa mwezzi (sawa na zaidi ya Sh. Mil. 800 kwa mwaka), matumaini yao ni kupandisha zaidi kiwango cha ufaulu wa sasa wilayani humo.

Shauri aliongeza ya kwamba, ukiondoa misaada ya wadau kama NMB na ruzuku ya Elimu Bure, eneo lingine wanalotegemea kupata pesa za kutatuzi changamoto za elimu na kukuza ufaulu, ni pamoja na asilimia 30 ya mapato ya ndani ya wilaya hiyo, iliyokamilisha ujenzi wa shule mpya 10 (tano za Msingi na tano za Sekondari).

Naye Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Mchemba, alisema kuwa kwa sasa wananachi wa wilaya hiyo wamepunguza kasi ya kupiga simu kwake na kutoa malalamiko juu ya huduma mbovu zilizokuwa zinatolewa na wahudumu wa Kituo cha Afya Gairo, tuhuma walizokuwa wakipata kwa miaka mitatu sasa kutoka kwa jamii.

Akizungumza wakati wa kupokea msaada kutoka NMB, Mchemba alisema kuwa, kwa sasa baada ya kukaa na watumishi hao hali imeadilika na inaweza kupita mwezi mmoja bila kupigiwa simu na wananchi kutoa malalamiko juu ya huduma zisizo bora na bila shaka mambo yamebadiliko kituoni hapo.

Aidha, Meneja Mahusiano na Biashara za Serikali, Kanda ya Mashariki wa Benki ya NMB, Anneth Kwayu, alisema kuwa Kituo cha Afya Gairo kimekuwa kikipokea vifaa mbalimbali kutoka NMB kwa miaka mitatu mfulilizo, katika jitihada za benki hiyo kusaidia kupunguza changamoto za afya.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Urambo, Angelina Kwingwa, akizungumza mapema jana kabla ya kupokea vitanda saba na mashuka ishirini na tano vyote vikiwa na jumla ya shilingi milioni tano kutoka benki ya NMB,ameipongeza benki hiyo kwa kupunguza adha za wagonjwa hasa wajawazito na watoto waliokuwa wakilala wawili hadi wanne kitanda kimoja.

No comments:

Post a Comment

Pages