June 14, 2019

TFDA YATOA ELIMU YA USALAMA WA CHAKULA KWA WAANDISHI WA HABARI

 Kaimu  Mkurugenzi Mkuu wa  TFDA, Adam Fimbo.
 
 
Na Asha Mwakyonde

MAMLAKA ya Dawa na Chakula Tanzania (TFDA), imesema kuwa imeweka mfumo thabiti  wa udhibiti kwa lengo la kuhakikisha chakula kinachozalishwa ndani ya nchi na kile kinachoingizwa kinakidhi vigezo vya usalama na ubora ili walaji wasipate  madhara kiafya.

Pia wanahabari wametakiwa kuwa mabalozi wa kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa masuala ya usalama wa Chakula.

Haya yalisemwa Wilayani Bagamoyo Pwani na Kaimu  Mkurugenzi Mkuu wa  TFDA, Adam Fimbo  wakati wa ufunguzi wa semina ya kuelimisha wanahabari kuhusu masuala ya usalama wa chakula.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa madhara mengi yatokanayo na chakula kisicho salama huchangiwa kwa kiasi kikubwa na uelewa mdogo wa jamii juu ya masuala ya usalama wa chakula  na kutozingatia ipasavyo kanunu za upatikanaji chakula salama.

Alitolea mfano baadhi vinasababishwa na uelewa mdogo miongoni mwa jamii kuwa ni uandaaji wa chakula katika mazingira yasiyo safi, kutonawa mikono kwa maji safi na sabuni baada ya kutoka chooni, kabla ya kuandaa chakula.

"Kwa mantiki hii elimu kwa umma juu ya kuhakikisha usalama wa chakula  katika hatua mbalimbali  za mnyororo wa chakula ni muhimu  katika kuleta mabadiliko chanya," alisema Fimbo.

Aliongeza kuwa kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), takimwimu zinaonesha takribani watu milioni 600 sawa na mtu mmoja kati ya 10 huugua kila mwaka kutokana na kula Chakula kisicho salama.

Mkurugenzi Fimbo alifafanua kuwa kati yao 420,000 hufariki na kwamba  kati ya hao watoto ni 125,000 wenye umri chini ya miaka mitano.

Kwa upande wake  Mkaguzi Mkuu wa  chakula kutoka mamlaka hiyo, Lazaro Mwambole alisema kuwa tayari TFDA ilishawafikia wajasiriamali  1500 kwa kutoa elimu juu ya masuala ya usalama wa Chakula katika mikoa mitano.

Alisema mwaandaji wa chakula kabla hajaanza kuandaa anatakiwa kupimwa Afya na kwamba wenngi wao wanaogopa kupima wakidhani wanapimwa ukimwi ndio maana huogopa.

"Changamoto kubwa iliyopo kwa waandaaji wa chakula baadhi yao wanatabia ya kuongea sana, kujikuna wakati kuundaa Chakula,"alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages