June 12, 2019

Uvivu wa Vijana wa Kiume Mkoani Rukwa wamkasirisha RC Wangabo

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo (mbele), akikagua ujenzi wa jengo la Wazazi katika hospitali mpya ya wilaya ya Nkasi.
 
 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo, amesikitishwa na uvivu wa kutofanya kazi kwa vijana wa kiume katika mkoa hali inayopelekea miradi mingi inayotekelezwa na serikali katika mkoa huo kwa kutumia force account inafanywa na vijana wanaotoka nje ya mkoa huo jambo ambalo sio madhumuni ya serikali ya awamu tano.

Amesema kuwa lengo la ujenzi kwa kutumia force account ni kuhakikisha kwamba wananchi wa maeneo husika wanapata manufaa ya ujenzi ule na kufanya ujenzi huo kuwa ni wa kwao na kujivunia kwamba walishiriki tangu mwanzo wa ujenzi huo kuanzia ngazi ya songambele ya kuchimba msingi hadi kumalizika kwa majengo hayo

“Watu wameshiriki kweny songambele hapa lakini baadae tunapotafuta vibarua wa kufanya kazi, mtu anafanya siku mbili, siku tatu akipewa malipo yake anapotea, Uvivu, sasa hii tabia ya uvivu hii ndio ambayo ningependa kutoa wito kwa wananchi wangu ndani ya mkoa wa Rukwa kuwa waache uvivu, mbona kuna mabinti na kina mama wanachapa kazi kule, hawakimbii wanapiga kokoto na wako wengi, lakini vijana wa kiume wanataka kupiga draft, kufanya vitu vyepesi vyepesi, hii tabia ningewaasa waiache,” alisema

Ameongeza kuwa kwa kufanya hivyo miradi hivyo wanakosa umiliki wa miradi hiyo na kuiona ni miradi isiyowahusu na hivyo kuwataka wananchi kujitokeza katika ufundi na vibarua ili kufanye kazi na kujipatia kipato na kuacha uvivu.

Ameyasema hayo alipotembelea ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Nkasi inayojengwa katika mji mdogo wa Namanyere wilayani humo akiongozana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa pamoja na wataalamu kutoka katika ofisi ya mkuu wa mkoa.

Katika ziara hiyo Mh. Wangabo amepongeza hatua iliyofikiwa katika ujenzi huo unaoendelea huku majengo yote saba ya hospitali hiyo yakiwa yamefikia katika hatua ya kupaua na kuzingatia ubora katika ujenzi huo huku vifaa vyote kwaajili ya ujenzi huo vikiwa tayari vimeshanunuliwa na kuwaasa kuwa hadi kufikia tarehe 30.6.2019 wahakikishe mafundi wanakabidhi majengo hayo kwaajili ya kuanza kutumika.

Mmoja wa vibarua anaetokea mkoa wa shinyanga, Joseph James kwa niaba ya wenzie alisema kuwa tangu wafike hapo wamekuwa wakilipwa vizuri na wanaona kuwa kazi zinakwenda sawa na hawana malalamiko yoyote huku fundi wao mkuu katika jengo la maabara alikiri kuwa vibarua wake anawatoa mkoa wa shinyanga na kuwa vijana waliopo katika wilaya ya Nkasi ni wavivu na walikuwa wakirudisha nyuma kasi ya kazi.

Awali akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa hospitali hiyo Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Said Mtanda alisema kuwa ujenzi huo unakwenda kwa awamu tatu na hadi kufikia tarehe 15.6.2019 awamu ya kwanza itakuwa imeisha na awamu ya pili ya kupaka majengo rangi pamoja na kuweka fremu za milango na madirisha tayari imeshaanza kufanyika na awamu ya mwisho ni kuweka marumaru kwenye majengo yote hivyo hadi kufikia tarehe 30.6.2019 ujenzi huo utakuwa umekamilika.
 
“Kwa zote hadi sasa tumeshatumia kama shilingi bilioni 1.15 na mpaka jana kweny akaunti tuna kama shilingi milioni 351 ambazo matarajio yetu ni kwamba zitakidhi shughuli za mradi kwasababu kwa upande wa mafundi wote wameshalipwa haki zao kitu ambaco kimebakia katika kununua ni masuala ya marumaru na kulipia aluminiam ya vioo na kumalizia kuwalipa mafundi wakaofanya kazi awamu ya pili, matarajio yetu fedha hiyo itakidhi mahitaji hayo,” Alimalizia.

No comments:

Post a Comment

Pages