June 12, 2019

Mkaa endelevu waondoa utegemezi Matuli, Mlilingwa

 Mwenyekiti wa Kijiji cha Matuli, Salum Mrisho akielezea mradi wa ujenzi wa choo cha Shule ya Msingi Matuli kwa maofisa misitu, maliasili, kilimo, ardhi, sheria na maendeleo ya jamii waliotembelea kijiji hicho mradi huo umefadhiliwa na Kijiji kwa fedha zilizotokana na mradi wa mkaa endelevu.
 Mratibu wa Misitu ya Asili Tanzania, Emmanuel Msofe, akizungumza na wanakijiji na maofisa wa serikali waliokuwa wametembelea Kijiji cha Matuli kujifunza kuhusu mradi wa mkaa endelevu.
 Mchoma Mkaa wa Kijiji cha Matuli, Ashura Rajab akielezea kwa maofisa, maliasili, misitu, kilimo, ardhi, sheria na maendeleo ya jamii ambao walifanya ziara ya siku tatu kujifunza kuhusu mradi wa mkaa endelevu.

 
Na Suleiman Msuya

MRADI wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS), maarufu 'Mkaa Endelevu' umefanikiwa kuondoa utegemezi kwa wakina mama na wananchi wa vijiji vya Matuli na Mlilingwa wilayani Morogoro mkoani Morogoro.

 Ushuhuda wa wakuondokana na utegemezi umetolewa na wanakijiji hao wakati wakizungumza na mwandishi wa habari hii ambaye alikuwa katika ziara ya siku tatu iliyoandaliwa na TTCS kwa maofisa misitu, maliasili, ardhi, kilimo, sheria na maendeleo ya jamii kutoka wilaya 16 nchini.

Akizungumzia mradi huo Ashura Rajab alisema tangu kuanzishwa mradi huo wanawake wamekuwa wakijiamini na kuhudumia familia yao na kuchana na utegemezi.

Rajab alisema awali wanawake walikuwa wanajishughulisha na kilimo cha mazao ya chakula kisicho na tija ila kwa sasa wamefanikiwa kujikita na kilimo cha kisasa, uwekaji hisa na uchomaji mkaa kwa njia endelevu hivyo kujiongezea kipato.

"Miaka ya nyuma tulikuwa tunategemea kila kitu kwa wanaume zetu ila kwa sasa tunakaa tunajadili maendeleo kwa pamoja," alisema.

Kwa upande wake Mchoma Mkaa Aisha Juma, alisema mradi umefanikisha kusomesha watoto wake bila kutegemea mtu.

Alisema awali alikuwa anajikimu kwa kufanya vibarua vya kulima ambavyo vilikuwa havimlipi ila kwa sasa mkaa endelevu umemuwezesha kufanya makubwa.

"Mimi nilikuwa najihusisha na kazi za vibarua vya kilimo ambapo ilikuwa hakilipi ila kusema kweli mkaa endelevu umenikomboa watoto wanasoma vzuri, nimemalizia nyumba yangu na nitaanza kufanya biashara baada ya kuuza mkaa huu," alisema.

Salima Shaban Muhasibu wa Kikundi cha Wakata Mkaa Kijiji cha Mlilingwa, alisema mradi umesaidia upatikanji wa huduma za afya kwa urahisi hivyo kuondoa kero kwa familia.

"Mradi umetusaidia sana kwani nafaya biashara, nakopesheka lakini pia usawa umeongezeka ndani ya nyumba, naomba Serikali iangalie namna ya kuendeleza mradi huu," alisema.

Naye Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Matuli, Cosmas Kadebe, alisema kwa zaidi ya miaka 50 kijiji hicho kimekuwa nyuma kimaendeleo ila miaka mitatu ya TTCS imefanya mapinduzi ya kiuchumi, kijamii na maendeleo.

"Mradi huu ni mkombozi mkubwa ndani ya kijiji kwani miaka yote tulikuwa tunagombana wanakuja wavamizi wanakata misitu ila TTCS imetufungua na tunafaidi," alisema.

Kwa upande wake Ali Rajab aliomba mradi huo kuwa endelevu kwa kuwa unasaidi serikali kutatua changamoto nyingi kama elimu, afya, miundombinu, kilimo na nyinginezo.

Diwani wa Kata ya Matuli, Lucas Lemomo alisema, mradi huo umemrahisishia kufanya kampeni 2020 iwapo chama chake kitampitisha kugombea.

Lemomo alisema kupitia mradi huo ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 1 hadi 99 ambapo mwaka 2017 wanafunzi 49 wa Shule ya Msingi Matuli walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kati 53 waliomaliza.

"Mwaka jana wanafunzi wote 25 walichaguliwa na sababu ni kambi ya masomo iliyofadhiliwa na fedha za kijiji zilizotona na mradi wa mkaa endelevu," alisema

Alisema ufaulu huo umechangia kijiji kuanza mchakato wa kujenga shule ya sekondari ambayo itasaidia kupunguza safari kwa wanafunzi kufuata shule kata ya Ngerengere.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Matuli Salum Mrisho,  alisema mkaa endelevu umefanikisha ujenzi wa matundu 24 ya choo shule ya msingi Matuli na madarasa mawili.

Mradi wa TTCS, unatekelezwa na Shirika la Kuhifadhi, Misitu ya Asili Tanzania (TFCG, Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (Mjumita) na Shirika la Kuendeleza Nishati Asili Tanzania (TaTEDO) chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswis (SDC).

No comments:

Post a Comment

Pages