June 11, 2019

WAZIRI UMMY KUPELEKA MUSWADA BUNGENI WA KUWATAKA WAENDESHA PIKIPIKI KUWA NA BIMA YA AFYA KABLA YA KUPEWA LESENI

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia,Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
 
Na Asha Mwakyonde

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia,Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema anatarajia kupeleka muswada bungeni wa dereva atakayeendesha pikipiki kabla ya kupewa leseni awe na bima ya afya kwanza.

Alitaja sababu ya kutaka kupeleka muswada huo bungeni ni kutokana na ajali zitokanazo na pikipiki kuwa nyingi na kusababisha gharama za matibabu kwa sekta ya afya kuwa kubwa.

Akizugumza jijini Dar es Salaam leo, wakati wa ufunguzi wa kambi ya utoaji wa miguu bandia kwa kwa watu 600 katika taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Waziri Ummy alisema taasisi hiyo kwa mwezi imekuwa ikipokea wagonjwa 700 hadi 900 wa ajali za pikipiki.

Ummy alisema idadi hiyo ni kubwa na imekuwa ikiongezeka kila siku kwa sababu awali taasisi hiyo ilikuwa ikipokea wagonjwa wa ajali hizo 400 hadi 600 kwa mwezi.

“Nimeongea na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na kumuomba waangalie jinsi ya kuzidhibiti pikipiki hizo kwani zimekuwa zikibeba zaidi ya abiria wawili hadi watatu,hivyo nimemuomba kabla dereva bodaboda hajapewa leseni sharti la kwanza awe na bima ya afya ndio apatiwe leseni yake ya udereva,”alisema.

Alisema  ni vyema kila mtu akawa na bima ya afya kwa sababu gharama za upasuaji pindi mtu apatapo ajali ni kubwa, Taasisi ya MOI gharama za upasuaji mdogo ni sh. 200,000 na ili mtu apatiwe mguu ni sh. milioni 1.5 hadi tatu.

Vilevile Ummy alisema  katika kambi ya upimaji wa watu wanaotakiwa kupatiwa miguu bandia waliojiandikisha walikuwa 900 na waliofanikiwa kupewa miguu hiyo ni 600 hivyo aliwaahidi kuangalia namna ya 300 waliobaki kupatiwa miguu hiyo.

“Zoezi hilo limefanikiwa kwa kushirikiana na Ubalozi wa China ambao umekuwa mstari wa mbele kuchangia sekta ya afya ambapo mwaka jana walichangia dawa zilizokuwa na thamani ya sh.bilioni mbili na wameahidi tena kutoa  fedha hizo mwaka huu ambapo dawa za sh.milioni 500 watapewa MOI,”alisema.

Alisema ameona dawa za sh.milioni 500 kupewa MOI kwa sababu amekuwa akiridhika na huduma zinazotolewa katika taasisi hiyo japo ya kuwa na baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo.

Hata hivyo aliwaahidi MOI kuwa serikali itahakikisha inatatua changamoto zilizopo kwa wakati.

Naye Mwenyekiti wa Bodi wa MOI, Charles Mkonyi, alimshukuri Raisa Dk. John Magufuli kwa kuwezesha upatikanaji wa huduma,kufunga vifa vya kisasa vya uchunguzi.

“Mafanikio ya MOI, Rais Dk. Magufuli ndio muasisi wa ushirikiano uliopo kati ya taasisi hiyo na serikali ya China,hivyo tunamuomba Waziri Ummy kusaidia upanuzi wa eneo la mazoezi kwa sababu kwa sasa kumekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages