Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk. Angeline Mabula,
akizungumza na Mmiliki wa shule za Musabe zilizoko mkoani Mwanza Daniel Musabe
wakati wa oporesheni ya kufuatilia wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi
katika mkoa wa Mawanza mwishoni mwa wiki. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Kitengo
cha Kodi Wizarani Denis Masami na wa tatu kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa shule
za Musabe Faustine Magabilo. (Picha na Wizara ya Ardhi).
Na Munir Shemweta, WANMM MWANZA
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi amezidi kuzibana Taasisi na Makampuni yenye
madeni makubwa ya kodi ya pango la ardhi ambapo ametua mkoani Mwanza na
kuyabana makampuni na taasisi nane ambazo kwa ujumla wake zinadaiwa zaidi ya milioni
900.
Kampuni na taasisi
alizotembelea Dkt Mabula ni Synergy Tanzania Ltd, Ideal Development Ltd,
Birchard Oil Ltd, Shule za Musabe, Taasisi ya Taifa ya Utafiti Magonjwa ya
Binadamu (NIMR), Ndamavyo Auto Spares, Jesse & Company Ltd na Maabara ya
Taifa ya Udhibiti Samaki na Mazao ya Uvuvi.
Akizungumza katika
ziara yake hiyo ya kufuatilia madeni ya kodi ya pango la ardhi mwishoni mwa
wiki, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema ziara hiyo
anayoifanya ya kuwafikia wale wenye madeni makubwa inafuatia baadhi ya kampuni
na taasisi zinazodaiwa kushindwa kulipa ama kurekebisha madeni yao baada ya
kikao cha Juni 11, 2019 kilichowakutanisha wadaiwa zaidi ya 200 jijini Dodoma
katika mwanzo wa ziara
yake kwenye shule za Musabe, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi alimueleza mmiliki wa shule hizo Daniel
Musabe kulipa deni lake la kodi ya pango la ardhi linalofikia milioni 57.4
katika viwanja vyake vinne anavyomiliki kufikia tarehe 31 Julai 2019 ili
kuepuka kufikishwa katika Baraza la Ardhi na Nyumba.
Hata hivyo, Mmiliki wa
Shule hizo ambazo ni za Chekechea, Msingi na Sekondari alimueleza Dkt Mabula kuwa
yuko tayari kulipa deni la kodi ya pango la ardhi lakini alishindwa kufanya
hivyo kutokana na changamoto za kibiashara ambapo hata hivyo aliahidi kulipa
kiasi anachodaiwa kuanzia Agosti 2019 na kumaliza deni lote ifikapo Desemba
2019.
Akiwa katika Kampuni ya
Birchard Oil Limited, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt
Mabula ambaye aliambatana na Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizarani Denis Masami aliitaka
kampuni hiyo kulipa kiasi inachodaiwa cha kodi ya pango la ardhi inayofikia
milioni 85,235,050 ikiwa ni pamoja na malimbikizo ya kodi za miaka ya nyuma.
Meneja uhusiano wa Kampuni
hiyo inayojishughulisha na uzalishaji Mafuta na Marobota ya Pamba Arshad Jetha
alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi kuwa kampuni yake pamoja na kudaiwa kodi ya
pango la ardhi kwa baadhi ya viwanja inavyomiliki lakini baadhi yake
alishalipia hivyo aliomba kuhakikiwa madeni yake ili kupata deni halisi.
Ideal Development Ltd
kupitia Meneja wake Burnanuddin Rajbhai alikiri deni la kodi ya pango la ardhi
linalofikia milioni 79 na kuomba kupewa muda wa kulipa katika awamu tatu
tofauti. Hata hivyo, Naibu Waziri wa Ardhi alizitaka kampuni na Taasisi
zilizokubali kulipa madeni kuandika
barua ya kueleza namna zitakavyolipa na muda wa mwisho wa kulipa madeni yao katika
ofisi za ardhi za halmashauri husika na nakala za barua hizo ziende ofisi ya
Kamishna Msaidizi wa Ardhi wa Kanda ya Ziwa.
Kamishna Msaidizi wa
Ardhi Kanda ya Ziwa Makwasa Biswalo aliionya kampuni ya Ideal Development Ltd
kwa kushindwa kutekeleza makubaliano yaliyofikia ya kulipa deni lake na
kuieleza kuwa hatua itakayofuata kwa kampuni hiyo ni kufikishwa katika Baraza
la Ardhi na suala la kuingia makubaliano ya malipo haliwezi kufanyika kwa mara
ya pili.
Kampuni ya Synergy
Tanzania Ltd Kupitia kwa Meneja Utawala wake Florence Kivamba iliahidi kuandika
barua ya makubaliano ya kulipa deni la milioni 43 inayodaiwa ingawa alioamba
kufanya mawasiliano na uongozi wa juu kwa kuwa ziara ya Naibu Waziri wa Ardhi ilikuwa
ya kushtukiza na uongozi haukuwepo.
Akiwa katika Taasisi ya
Taifa ya Utafiti Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Mabula
aliueleza uongozi wa Taasisi hiyo kuwa inadaiwa jumla ya shilingi milioni 515,713,900
ya kodi ya pango la ardhi na taasisi hiyo haijawahi kulipa kodi hiyo tangu
mwaka 1996.
Mkurugenzi wa NIMR mkoa
wa Mwanza Safari Kinuhi alijitetea kwa kueleza kuwa taasisi yake inapaswa
kusamehewa kulipa kodi ya pango la ardhi kwa kuwa haiko kibiashara bali inatoa huduma
kwa wananchi na kuboresha afya ingawa aliahidi kuwasiliana na uongozi wa juu
kuhusiana na suala hilo.
Hata hivyo, Dkt Mabula
alimueleza kuwa Taasisi yake inapaswa kufuata sheria wakati wa kuomba
kusamehewa kodi ya pango la ardhi huku Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizarani Denis
Masami akisisitiza kuwa hata kama Taasisi hiyo itasamehewa kulipa kodi hiyo
lakini deni la nyuma lazima lilipwe kwa kuwa sheria ya msamaha itaanza pale
tamko la msamaha lilipotoka.
Maabara ya Taifa ya
Udhibiti Samaki na Mazao ya Uvuvi iliyopo eneo la Nyegezi ilionekana kutokuwa
na hati ya eneo inalomiliki ingawa Afisa Mfawidhi wa Taasisi hiyo Emanuel
Mundoko alijitetea kwa kueleza kuwa awali Taasisi hiyo ilikuwa sehemu ya chuo
cha Uvuvi na sasa inajitegemea hivyo hawajui madeni halisi wanayodaiwa.
No comments:
Post a Comment