July 14, 2019

Denti miaka 14 awagaragaza ‘Wahenga’ riadha Majimaji Selebuka 2019

Katibu Tawala Wilaya ya Songea, Upendo Ndumbaro akikabidhi zawadi kwa mshindi wa pili wa mbio za mita 400, Alto Lwena, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Luwawasi katika tamasha la wiki nzima la Majimaji Selebuka 2019 linaloendelea Uwanja wa Majimaji, Songea.

Mkuu wa Wilaya ya Songea, Poreleti Kamando, akimvisha medali ya fedha, Vailet Kidasi (Njombe) aliyemaliza wa pili katika mbio za 5KM kwa wanawake katika tamasha la Majimaji Selebuka 2019, zilizoandaliwa na Asasi ya Songea-Mississippi (SO-MI).

Keplin Kipili kutoka mkoani Mwanza, akihitimisha mbio za Mita 400 kwenye Tamasha la Majimaji Selebuka 2019 linaloendelea kwenye Uwanja wa Majimaji, Songea. Keplin aliibuka bingwa katika kategoria zote tatu alizoshiriki za Mita 200, 400 na KM 5.

Mkurugenzi Mwenza wa Taasisi ya Songea-Mississippi (SO-MI) ambao ni waratibu wa Tamasha la Majimaji Selebuka, Prof. Julian Murchison, akimkabidhi zawadi kinara wa mita 100 kwa wanaume, Shija Mohammed wa Shule ya Sekondari ya Mashujaa (Songea). Tamasha hilo linaendelea kwenye Uwanja wa Majimaji, Songea.

Mwenyekiti wa Tamasha la Majimaji Selebuka, Nathan Mpangala akitoa zawadi kwa mshindi wa tatu Mita 100 kwa wasichana, Fitina Omary wa Shule ya Msingi, Kisiwani.

Mkuu wa Wilaya wa Songea, Poreleti Kamando akimvisha medali ya dhahabu, bingwa wa mbio za 5KM kwa upande wa Walemavu, Shukuru Alfani kwenye Tamasha la Majimaji Selebuka. Nafasi ya pili ilichukuliwa na John Stephano.

Nathan Mpangala, mwenyekiti wa Tamasha la Majimaji Selebuka, akimpongeza bingwa wa mbio za Mita 100 kwa wasichana, Aida Manyai wa Shule ya Msingi Misufini katika mashindano ya riadha yaliyoandaliwa na Taasisi ya Songea-Mississippi (So-Mi). 
 
 
Na Mwandishi Wetu, Ruvuma
 
 MWANAFUNZI kutoka shule ya msingi Luwawasi mjini Songea Mkoa wa Ruvuma, Aveline Ndimbo (14), amewaacha midomo wazi umati wa wananchi waliojitokeza kushuhudia Tamasha la Majimaji Selebuka 2019, baada ya kutoa upinzani mkali kwa wanariadha wazoefu katika mbio za mita 200 kwa wasichana.

Katika mbio hizo zilizofanyika kwenye Uwanja wa Majimaji, Aveline alishika nafasi yapili akitumia sekunde30.67 akitanguliwa Keflin Kipili wa Mwanza 27.74 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Vailet Kidasi kutoka Njombe 32.03.

Keflin na Vailet ni wanariadha waliowahi kushiriki mashindano mbalimbali nchini, tofauti na Aveline.
Mita 200 wavulana mshindi aliibuka Abonto Abonto wa Sekondari ya Kiislamu ya Songea aliyetumia sekunde 25.56 akifuatiwa na Hamis Rajab wa Sekondari ya Londoni 26.10 na nafasi ya tatu kwenda kwa Batromeo Kilangazi kutoka Ajuco 26.48.

Kwenye mita 100 wasichana mshindi aliibuka Aida Manyai kutoka Shule ya Msingi Misufini aliyetumia 14.66 akifuatiwa na Amina Juma wa Mashujaa Shule ya Msingi 15.30 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Fitina Omar wa Kisiwani 16.75.
Mita 100 wavulana mshindi ni Shija Mohamed wa Mashujaa sekunde 12.51 akifuatiwa na Bushir Ally wa Majimaji sekunde 13.47 huku mshindi wa tatu akiibuka Daud Robert wa Mashujaa 13.97.

Katika mita 400 wasichana Keplin Kipili wa Mwanza alishinda akitumia dakika 1:05.93 akifuatiwa naVailet Kidasi wa Njombe 1:11.03 huku nafasi ya tatu ikinyakuliwa na Anastazia Kapinga Luwawasi Sekondari 1:18.98
Funga kazi ilikuwa kwenye mbio za barabarani Kilomita 5, ambako kwa wanaume Osca Kayombo kutoka Lilambo mjini Songea alishinda akitumia dakika 16:47.28 akifuatiwa na John Mahangula dakika 16:59.50 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Abibu Zidady wote wa mjini Songea dakika 17:01.48.

Kwa upande wa wanawake Kilomita 5 Keflin Kipili wa Mwanza aling’ara tena akitumia dakika 20:00.11 akifuatiwa na Vailet Kidasi wa Njombe 20:01.12 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Celina Tahan wa Songea 28:30.30.

Walemavu Kilomita 5, waliwa wawili ambako kinara aliibuka Shukuru Alfan aliyetumia dakika 20:53.41 akifuatiwa na John Stephano dakika 26:37.00 wote kutoka Dar es Salaam.

Tamasha hilo lilifunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Songea Poreleti Kamando aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mdeme, ambapo aliwapongeza waandaji wa tamasha, Taasisi wa SO-MI kwani limewainua wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kiuchumi na vipaji.

“Nimefurahishwa na huyu binti (Aveline) ameweza kuwashinda watu wazima tena maproshino ila amewashinda. Hili ni jambo jema la kujivunia kuwepo kwa tamasha la Majimaji Selebuka. Taarifa zake nimezipata na nitahakikisha nazifikisha kwa viongozi wa juu wa mchezo husika, ili vipaji hivi viendelezwe hasa kwa watoto wadogo,” alisema Mhe. Kamando  

Tamasha hilo la wiki nzima, limekata utepe Julai 13 na litafikia tamati Julai 20.

No comments:

Post a Comment

Pages