July 22, 2019

MAELEZO, XINHUA Wasaini Mkataba Kuimarisha Ushirikiano

 Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.Hassan Abbasi Kulia, na Mhariri Mkuu wa shirika la Xinhua Tanzania Si Sibo Li Kushoto, wakisaini mkataba wa Ushirikiano ,  waliosimama kutoka kulia  ni Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe, Katikati ni Bw.He Ping Mhariri Mkuu wa Xinhua na mjumbe wa Kamati Kuu ya  Chama cha CPC na Kushoto Wang Ke balozi wa China nchini Tanzania, wakishuhudia tukio hilo. (Picha na Idara ya Habari MAELEZO).
Kutoka Kushoto Balozi wa China nchini Tanzania Wang Ke, Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe, Mhariri Mkuu wa Xinhua na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha CPC He Ping, Dkt.Hassan Abbassi Mkurugenzi wa Idara ya Habari na MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, pamoja na Si Sibo Li Mhariri Mkuu wa Xinhua Tanzania , wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kusaini makubaliano Jijiji Dar es Salaam.
 


Na Mwandishi Wetu-MAELEZO

Ofisi ya Idara ya Habari MAELEZO chini ya Wizara ya Habari Utanaduni Sanaa na Michezo, imesaini Mkataba wa Ushirikiano kati yake na Shirika la Habari la Serikali ya China Xinhua ili kuimarisha na kukuza ushirikiano kati ya Tanzania na China ulioasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mao Tse Tung.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini Mkataba huo iliyofanyika Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe alisema ushirikiano wa Tanzania na China umekuwepo kwa miaka mingi katika Nyanja mbalimbali na sasa nchi hizo zimekua kama ndugu.

Waziri Mwakyembe alisema yapo mambo mengi yalioacha alama kwenye ushirikiano wa kindugu kati ya China na Tanzania, ikiwemo reli ya Tazara pamoja na uwanja mkubwa wa Taifa Jijini Dar es Salaam pamoja na majengo mbalimbali makubwa.

“Nafurahi kuona leo wenzetu wa Idara ya Habari Maelezo wanatiliana saini mkataba wa ushirikiano kati yao na Xinhua, hii inadhihirisha kukomaa kwa urafiki kati ya Tanzania na China na imeongeza wigo wa maeneo ambayo nchi hizi mbili zinashirikiana” Alisema Waziri Mwakyembe.

Alisema licha ya kwamba kuna mashirika ya Habari ya China ambayo yanafanya kazi hapa nchini kama CCTV,CGTN,  XNHUA pamoja na baadhi ya magazeti, ushirikiano mpya uliosainiwa kati ya Xinhua na Idara ya Habari Maelezo utaimarisha zaidi sekta ya habari hapa nchini , na pia utasaidia kubadilishana uzoefu katika masuala ya habari na mawasiliano kwa ujumla.

Kwa upande wake mhariri Mkuu wa Shirika la Xinhua ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya chama cha ukombozi cha watu wa China CPC Bwana He Ping, alisema amekuja Tanzania kuimarisha uhusiano wa kindugu ulioasisiwa na waanzilishi wa mataifa haya mawili, na pia kushuhudia utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya Idara ya Habari Maelezo na shirika la Habari la Xinhua.

Alisema tangu mwaka 1969 Xinhua imekua ikileta wanahabari wake kufanya kazi hapa nchini, lakini ushirikiano mahsusi kama ulioanzishwa kati ya Shirika hilo na Idara ya Habari, utasaidia katika upatikanaji wa  habari nyingi za maendeleo kwani nchi yake inahangaika usiku na mchana kuendelea kuwaletea wananachi wake maendeleo.

“Lengo letu kama taasisi ya Serikali ni moja tu kuhakikisha kwamba habari tunazoandika na kusambaza zinachangia katika kuboresha maisha ya wananchi kwa kujikita hasa katika habari za maendeleo, hili linatakiwa kusisitizwa sana kwani katika miaka 40 iliyopita China ilikua ni nchi inayoendelea lakini kwa sasa imepiga hatua kubwa za maendeleo duniani” Alisema Bwana Ping.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.Hassan Abbasi, alisema habari ni maendeleo na ushirikiano huo ulioanzishwa utaendelea kuleta chachu ya maendeleo baina ya Tanzania na China hasa katika kipindi hiki ambacho Tanzania inafanya mageuzi makubwa.

“Sisi tuko tayari kuwapa habari za kina na zenye takwimu sahihi ili mtusaidie kuieleza dunia kwamba Tanzania sasa tunapiga hatua, kama mlivyofanya mageuzi makubwa ya kiuchumi huko China na sisi tunajitahidi kuhakikisha tunakua Taifa lenye maendeleo makubwa na lenye nguvu kiuchumi” Alisema Dkt Abbasi.

Mkataba uliosainiwa kati ya Idara ya Habari MAELEZO na Shirika la Xinhua una lengo la kuimarisha uhusiano  katika kubadilishana habari na taarifa mbalimbali, kupitia magazeti na majarida lakini pia kupitia mitandao ya kijamii.

Aidha katika Ushirikiano huo Idara ya Habari Maelezo italisaidia shirika la Xinhua katika kupanga na kufanya mahojiano na viongozi wa serikali, Taasisi na wakala mbalimbali pamoja na kuwawezesha waandishi wa Shirika hilo kufanya kazi zao kwa wepesi zaidi hapa nchini.

Katika mkataba huo wa ushirikiano Idara ya habari pia itawasaidia waandishi wa habari wa Xinhua katika kupata vibali vya kufanyia kazi hapa nchini pamoja na kuwapatia vitambulisho vya wanahabari (Press cards).

Kwa upande wa shirikala Xinhua watasaidia kwenye kutafiti,kuandika na kutoa habari ambazo zinaisaidia Serikali kupitia Ofisi ya Msenaji Mkuu, pia watahakikisha habari wanazotoa zinz viwango vinavyokubalika na Idara ya Habari, pamoja na kusaidia ujenzi wa kituo cha wanahabari  (press Center) Jijini Dodoma.

Utiaji saini wa mkataba huo wa ushirikiano, ulifanywa na Dkt.Hassan Abbasi Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali na Bwana Si Sibo Li ambaye ni mhariri Mkuu wa shirika la Xinhua hapa nchini.
Hafla ya utiaji saini mkataba huo wa ushirikiano, ulihudhuriwa pia na Balozi wa China hapa nchini Wang Ke, wawakilishi wa Xinhua kutoka Nairobi Kenya, wawakilishi kutoka Makao Makuu China, wawakilishi wa Idara ya habari Maelezo, Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo pamona na mwakilishi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

No comments:

Post a Comment

Pages