July 22, 2019

Wanariadha Filbert Bayi wafanyiwa tafrija nzito

Wanafunzi wa shule ya sekondari ya Filbert Bayi wakiwa
katika picha ya pamoja na vyeti vyao walivyokabidhiwa
juzi wakati wa hafla ya kuwapongeza kwa kuuwezesha
mkoa wa Pwani kutwaa ubingwa wa jumla wa mchezo wa
riadha katika Michezo ya Shule za Sekondari Tanzania
(UMISSETA) hivi karibuni. (Na Mpigapicha Wetu).


Na Mwandishi Wetu, Kibaha

SHULE za Filber Bayi (FBS) zimewafanyia tafrija nzito
wanariadha wake waliofanya vizuri na kutwaa ubingwa wa
jumla katika mchezo wa riadha katika Michezo ya Shule
za Msingi Tanzania (UMISSETA) iliyofanyika mkoani
Mtwara hivi karibuni.

Katika hafla hiyo ya chakula cha mchana iliyofanyika
katika ukumbi wa shule hizo uliopo Mkuza, Kibaha,
wanariadha hao walitwaa medali 14 za dhahabu, mbili za
fedha na mbili za shaba, walipongezwa na kukabidhiwa
vyeti.

Mkurugenzi Mkuu wa shule hizo, Anna Bayi alisema kuwa
wanafunzi hao ambao wanasomeshwa bure katika shule
hiyo, wamefanya jambo kubwa katika mkoa wa Pwani kwa
kuuwezesha kushika nafasi ya kwanza katika riadha, licha
ya uongozi wa mkoa kukaa kimya.

Aliwapongeza vijana hao kwa matokeo mazuri ya
Umisseta na kusisitiza kuwa siri ya mafanikio na
maandalizi mazuri licha ya changamoto zilizokuwepo za
wilaya kushindwa kufuata utaratibu wa kuwachukua
wanafunzi kuwapeleaka katika mashindano ya mkoa.

Alisema baada ya mafanikio ya Kibiti, timu nzima
iliyoundwa na wanariadha wengi wa Filbert Bayi
ilichaguliwa kuunda timu ya mkoa na kwenda kushindana
Mtwara katika Michezo ya Umisseta Taifa, ambako nako
walipasua.

Filbert Bayi pekee katika mashindano hayo ya taifa
walitwaa medali 18, kitu ambacho sio kidogo na ndio
maana waliamua kuwapongeza kwa hafla hiyo, ambayo
inawafanya watoto kujiona kuwa wanatambulika.

Alisema mbali na kung’ara katika michezo, Bayi alisema
pia kuwa wachezaji hao ni tishi pia katika taaluma na sio
kweli kuwa wachezaji hawana uwezo michezoni,
kinachotakiwa ni kupanga ratiba nzuri ya masomo na
michezo.

Alisema kuwa hakuna mtu asiye na uwezo ila
kinachotakiwa ni juhudi na malengo ya kufanya vizuri
katika michezo mbalimbali.

Aliwataka viongozi wa mikoa kuwapongeza watoto
wengine walioshiriki michezo ya Umisseta ili kuwatia moyo
hata kama hawajarudi na medali, kikubwa ni kuwapokea na kuwapa pole kwa kushiriki na kufanya vizuri katika
michezo hiyo.

Alisema mwakani watawafanyia sherehe wachezaji wa
michezo yote watakaoshiriki Umisseta kutoka mkoa wa
Pwani hata kama uongozi wa mkoa hauko tayari kufanya
hivyo.

Wanariadha wa shule za Filbert Bayi waliotwaa medali ni
Regina Mpigachai aliyepata medali tatu za dhahabu na
moja ya shaba, huku Gaudencia Maneno akitwaa medali
tatu za dhahabu, huku Benedicto Mathias alitwaa medali
mbili za dhahabu na moja ya fedha.

Wakati Helemengilda Nkulilei alipata medali mbili za
dhahabu na moja ya shaba wakati Pili Mipawa alipata
medali mbili za dhahabu, Amos Charles alipata medali
moja ya dhahabu na moja ya fedha huku Esther Martin
alitwaa medali moja ya dhahabu.

Pia katika hafla hiyo alikuwepo mwanafunzi wa shule ya
Kibaha Moses Chacha aliyepata meali ya dhahabu,
ambaye naye alikabidhiwa cheti cha shukrani kama
wengine wa Filbert Bayi.

No comments:

Post a Comment

Pages