July 11, 2019

MAKONDA ATENGA MAMILIONI YA FEDHA KWA WAANDISHI WA MITANDAO YA KIJAMII

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, akizungumza na waandishi wa mitandao ya Kijamii.
 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Waandishi wa habari wakiwa kazini.
 

Na Dotto Mwaibale

MAMILIONI ya shilingi yametengwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kama zawadi kwa ajili ya waandishi wa habari watakao shinda shindano la kuuliza maswali wananchi kuhusu Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Akizungumza ofisini kwake leo  Makonda alisema shindano hilo litawahusu waandishi wa habari wanao endesha mitandao ya kijamii, Online TV, Blog, Twitter, Website, Facebook na Instagram.

Alisema maswali yatakayoulizwa ni 12 ambayo yameandaliwa na ofisi yake ambapo mwandishi mshindi kwa kuuliza atajinyakulia kitita cha shilingi milioni tatu huku mwananchi atakayejibu vizuri atapata sh.100,000.

Alisema kuwa maswali mengine 12 yatabuniwa na waandishi wenyewe lakini yanatakiwa yawe yenye mvuto na kusisimua na mshindi wa eneo hilo atajinyakulia milioni tatu na mwananchi atakaye yajibu kiufasaha atapata sh.100,000.


"Maeneo litakapofanyika shindano hili ni sehemu za Bar, Saluni, kwenye vijiwe vya waendesha bodaboda, masokoni na kwa wamachinga ambapo waandishi watawauliza maswali mbalimbali ya jinsi wanavyoijua SADC na watakaojibu kwa usahihi watajinyakulia kiasi hicho cha fedha" alisema Makonda.

Alisema baada ya mahojiano hayo kila mwanahabari atayarusha hewani kwa kutumia mtandao wake.

Makonda alisema mshindi wa kwanza wa shindano hilo atapata sh.milioni tatu, mshindi wa pili milioni mbili na mshindi wa tatu milioni moja na kuwa sherehe ya kukabidhi fedha hizo kwa washindi itafanyika Agosti 5 mwaka huu katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa.

Shindano ili linafanyika ikiwa ni moja ya hatua ya hamasa kuelekea mkutano mkuu wa SADC ambao unatarajiwa kufanyika hapa nchini hivi karibuni ambao utaongozwa na Rais Dkt.John Magufuli.

No comments:

Post a Comment

Pages