July 11, 2019

MUHIMBILI YAPATA MSAADA WA MASHINE YA KISASA

Na Asha Mwakyonde

HOSPITALI  ya Taifa Muhimbili (MNH) imepata msaada wa machine ya kisasa ya Optical Coherence Tomography (OCT) ya kusaidia kupima magonjwa ya macho yenye zaidi ya thamani ya Shilingi milioni 100.

Mashine hiyo imetolewa na Shule ya Kwaya ya Westminister Cathedral  ya nchini Uingereza kupitia Hospitali ya  Mtakatifu Thomas iliyopo nchini humo kwa lengo la kusaidia wagonjwa wenye matatizo ya macho nchini.

 Mashine ya OCT inatumika kutambua magonjwa yaliopo katika pazia la macho (retina) kwa ajili ya kumsaidia daktari kuamua matibabu sahihi  kwa mgonjwa wa macho.

Akizungumza  wakati akikabidhi  mashine ya OCT, mwalimu wa kwaya ya watoto katika Shule ya Kwaya ya Westminister Cathedral  nchini Uingereza,
Matthew Wright  amesema watoto hao wenye umri kuanzia miaka minne hadi 13 wametoa kwa lengo la kusaidia  wagonjwa wenye matatizo ya macho nchini.

“Mashine ya OCT itasaidia kutoa matibabu kwa maelfu ya wagonjwa wanaohitaji huduma, huu ni mchango wa watoto wa Shule Kwaya ya Westminister Cathedral ambao wamechanga fedha zao ili kutoa msaada huu,” amesema  Mwalimu Wright.

Wright amesema mashine ya OCT pia itasaidia kutoa elimu kwa madaktari zaidi ya 20 wanaosoma jinsi ya kutoa matibabu kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa ya macho.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru baada ya kupokea msaada amemshukuru Mwalimu Wright pamoja na watoto waliochanga fedha za kununua machine ya OCT.

Prof. Museru amesema mashine hiyo itatoa mchango mkubwa kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na matatizo ya macho.

Hata hivyo ameahidi wataitunza ili iweze kufanya kazi kwa muda mrefu.

Aidha Prof. Museru amewataka wataalam kuhakikisha wanaitumia mashine ya  OCT kwa uangalifu ili iweze kudumu kwa mufa mrefu wakati wa kuchukua vipimo kwa wagonjwa.

No comments:

Post a Comment

Pages