July 20, 2019

NAIBU WAZIRI KANYASU AAGIZA TANAPA KUONDOA SINGLE ENTRY MAENEO YANAYOLALAMIKIWA KUDUMAA KIUTALII

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu akizungumza na Waoneshaji  kwenye ufunguzi wa Maonesho ya Utalii wa Utamaduni ya Serengeti  yanayofanyika wilayani Serengeti mkoani Mara. Wapili kulia ni Mkuu wa wilaya ya Serengeti Nurdin Babu akiwa na pamoja na viongozi wengine. (Picha na Wizara ya Maliasili na Utalii).
 Naibu Waziri wa Malasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu (wa tatu kulia) akiwa na Mbunge wa Serengeti, Mhe.Chacha  Ryoba ( katikati)  wakipewa maelezo na muuza vinyago ambaye ni miongoni mwa Washiriki wa Maonesho hayo ya Utalii wa Kiutamaduni huku akiwa ameshika kinyago alipokuwa akimuelezea ubora wa Kinyago hicho katika Maonesho ya Utalii wa Utamaduni ya Serengeti yaliyofunguliwa rasmi mkoani Mara. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Maonesho hayo, Joshua Nyansiri. 
Mku wa wilaya ya Serengeti, Mhe. Nurdin Babu  akizungumza na Waoneshaji  kwenye ufunguzi wa Maonesho ya Utalii wa Utamaduni ya Serengeti  yanayofanyika wilayani Serengeti mkoani Mara kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu kwa ajili ya kufungua maonesho hayo.
 
 
Na Mwandishi Wetu
 
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu ameiagiza Hifadhi za Taifa ( TANAPA) kupitia upya sheria ya tozo ya kiingilio kwa watalii wanapotoka nje ya Hifadhi  inayowalazimu kulipwa tena wanapoingia ndani ya Hifadhi maarufu kwa jina la Single Entry waiondoe kwenye maeneo yanayolalamikiwa kuwa imeua shughuli za Utalii kwenye  vijiji vinavyozunguka Hifadhi.

Aidha,Mhe. Kanyasu ameagiza TANAPA iangalie maeneo ambayo inadhani ni muhimu  kwa Single Entry iendelee kutumika  kuwa waweke mfumo wa kielektroniki wa utambuzi wa vidole ( Biometric Identity) utakaoweza kutumika kubaini udanganyifu endapo utafanyika.

Amesema mfumo huo utawalazimisha watalii kuweka kidole wakati wakiwa wanaingia na wakati wanapotoka nje ya Hifadhi.

Amesema hali hiyo itawasaidia Waongoza  watalii kutoka nje ya Hifadhi na Watalii wao kwa ajili kuzitembelea jamii zilizokaribu na Hifadhi na hivyo kuzisaidia jamii kunufaika moja kwa moja kupitia utalii wa kiutamaduni.

Hayo yamesemwa kupitia  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu wakati alipokuwa akifunga Maonesho ya 8 ya Utalii wa Utamaduni ya Serengeti mkoani Mara.

Amesema tangu kuanzishwa kwa Single Entry kumepelekea madhara makubwa kwa baadhi ya maeneo yaliyo karibu na Hifadhi za Taifa kudumaa  kiutalii.

Ameyataja  maeneo hayo yaliyokaribu na yaliyoathirika moja kwa moja kuwa ni ukanda wa Magharibi katika geti la Ndabaka katika Hifadhi ya Serengeti na katika  Hifadhi ya Ruaha.
 
Akizungumza kwenye ufunguzi wa Maonesho hayo, Kanyasu amesema maeneo yaliyoathirika zaidi kutokana na kuwepo kwa Single Entry ni yale maeneo ambayo hayajapitiwa na barabara kuu pamoja na viwanja vya ndege.

Ametaja sababu zilizopelekea  kufa kiutalii maeneo hayo kuwa watalii walio wengi hulazimika kukaa ndani ya Hifadhi hadi muda wa masaa 24 yanavyoisha bila kutoka wakikwepa gharama endapo watatoka.

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu alimueleza Naibu Waziri huyo  kuwa wilaya yake asilimia 80 ni eneo la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti hivyo kutokana na uwepo wa Single entry wilaya hivyo imeathirika sana kwa vile imekosa watalii wanaotembelea vijijini tofauti na ilivyokuwa mwanzo kabla ya kuanzishwa.

" Mhe.Waziri tunakuomba uliangalie suala  hili, utalii wa kiutamaduni uliosaidia kuajiri wananchi wengi umekufa kutokana na Single Entry" alisisitiza

Ameongeza kuwa  endapo itaondolewa itasaidia watalii kuweza kutoka nje ya Hifadhi kuembelea vituo vingi vya utalii ambavyo vipo nje ya Hifadhi.


Naye, Anaeli Kilemi aliyesoma risala mbele ya Waziri huyo amesema Single entry imewadidimiza wananchi wengi ambao walikuwa wamejiajiri kupitia utalii wa kiutamaduni, Hivyo anaiomba serikali itatue tatizo hilo.

No comments:

Post a Comment

Pages