Mchezaji Bora wa Michuano ya soka ya Tamasha la Majimaji Selebuka 2019, Iral Alex 'Neymar' wa timu ya Lizaboni Junior (kulia) akipongezwa na Mbunge wa Songea Mjini na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Damas Ndumbaro ambaye alikuwa mgeni rasmi katika fainali kati ya Lizaboni na Tigo Fc kwa Tigo kuibuka bingwa.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk.
Damas Ndumbaro (kushoto) akimkabidhi kombe, nahodha wa timu ya Tigo Fc,
Abdallah Hausi baada ya timu hiyo kuibuka bingwa kwenye michuano ya soka
ya Tamasha la Majimaji Selebuka 2019 kwa kuichapa Lizaboni Junior mabao
2-1 fainali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Majimaji, Songea.
Fowadi wa timu ya Lizaboni Junior Iral Alex (jezi namba 10),
akidhibitiwa kisawasawa na nyota wa Tigo Fc wakiongozwa na Goddy Manji
(jezi namba 7) katika mchezo wa fainali ya Michuano ya soka ya Tamasha
la Majimaji Selebuka na Tigo kuibuka bingwa kwa ushindi wa mabao 2-1.
Fainali ilipigwa kwenye Uwanja wa Majimaji, Songea ambapo tamasha
linaendelea kwa shughuli nyingine.
Mabingwa wa michuano ya soka ya Tamasha la Majimaji Selebuka, timu ya
Tigo Fc wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mbunge wa Songea na Naibu
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Damas
Ndumbaro aliyekuwa mgeni rasmi katika fainali hiyo.
Na Mwandishi Wetu, Songea
MASTAA mbalimbali wa Ligi Kuu (TPL), na Ligi Daraja la Kwanza
(FDL), wakiongozwa na kiungo wa zamani wa Yanga, Pato Ngonyani na Peter Mapunda
wa Mbeya City, wamekuwa gumzo kwenye michuano ya soka kwenye Tamasha la
Majimaji Selebuka 2019, ambapo wamefanikiwa kutwaa ubingwa wakiwa na timu ya
Tigo FC mjini hapa.
Tigo iliibuka mabingwa kwa kuilaza Lizaboni Junior mabao 2-1 katika
mchezo wa fainali uliopigwa Juzi (Jumamosi), kwenye Uwanja wa Majimaji mjini
Songea na kuondoka na kitita cha Sh. Milioni 1, medali, kombe na jezi seti moja.
Ngonyani ambaye amemwaga wino kukipiga na Maafande wa Polisi
Tanzania waliyopanda TPL msimu huu, Mapunda na Selemani Mangoma wote wa Mbeya
City sambamba na Abdallah Hausi anayekipiga Majimaji Songea ya FDL, walikuwa nguzo
muhimu katika timu yao ya Tigo kwenye michuano hiyo iliyoshirikisha jumla ya
timu 16.
Mshindi wa pili, Lizaboni Junior iliambulia kitita cha Sh.
700,000 wakati washindi wa tatu Ruhuwiko Sekondari walijinyakulia Sh. 500,000
baada ya kufanya kufuru kwa kuinyeshea Mateka Fc mvua ya mawe ya mabao 8-3.
Mbali na zawadi hizo, timu zote zilizofanikiwa kuingia hatua
ya nusu fainali zilizawadiwa seti ya jezi moja huku Tuzo ya Kipa Bora
ilinyakuliwa na Martin Shimba wa Tigo FC, Mchezaji Bora wa Michuano alikuwa Iral
Alex ‘Neymar jr’ wa Lizaboni Junior wote wakiondoka na Sh. 50 kila mmoja.
Timu yenye nidhamu iliibuka Small Kids waliozawadiwa Sh.
100,000, Tuzo ya Mfungaji Bora ilikwenda kwa John Chinguku na Neva Kaboma wote
kutoka Ruhuwiko Sekondari waliofungana kwa mabao matano huku mwamuzi bora
alikuwa Thabit Manyamba ambao kila mmoja alipozwa Sh. 50,000.
Katika fainali hiyo Mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Damas Ndumbaro, ambaye pia ni
Mbunge wa Songea Mjini.
Tamasha la Majimaji Selebuka hufanyika kila mwaka mjini
Songea likihusisha matukio mbalimbali ikiwamo michezo, ngoma za asili, midahalo
kwa wanafunzi wa sekondari, utalii wa ndani na maonyesho ya wajasiriamali.
No comments:
Post a Comment