July 14, 2019

Madiwani kuanzisha vijiji vipya vya TTCS USM

Na Suleiman Msuya

MADIWANI na watumishi wa  Halmashauri ya Morogoro mkoani Morogoro wamesema watatenga bajeti ili kupima vijiji na kuendeleza Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS) katika vijiji vipya.

Wawakilishi hao wa wananchi wametoa ahadi hiyo wakati wakifanya maazimio ya mkutano uliondaliwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu Asili Tanzania (TFCG), Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa
 Misitu Tanzania (Mjumita), Shirika la Kuendeleza Nishati Asili (TaTEDO) chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswisi ((SDC).

Diwani wa Kata ya Mukulazi wilayani Morogoro, Abeid Muyanga alisema mradi huo ni fursa ambayo haifai kuachwa kuendelezwa hivyo kuwata wataalam wa wilaya kushirikiana na wataalam wa TTCS kuendeleza kwa vijiji vipya.

Mukulazi alisema maendeleo yanahitaji ushirikiano zaidi hivyo ni vema madiwani wakashikamana wakati mradi ukielekea ukingoni.

"Kwa kweli miaka miwili na nusu ya uwepo wa mradi huu imekuwa ya mapinduzi kwa kila sekta hivyo ili kuepusha kurudi nyuma tunapaswa kushikamana na kuendeleza," alisema.

Kwa upande wake Diwani wa Tununguo, Ndonga wa Ndonga alisema mradi huo umesaidia miradi mingi ya maendeleo hivyo hakuna budi kuindeleza kwa ushirikiano.

"Kwangu Mlilingwa huduma za maji, umeme, afya, elimu na huduma nyingine zimeboreka na sababu kubwa ni USM kupitia mfumo wa TTCS," alisema.

Akichangia katika mkutano huo Diwani wa Kolelo Eridius Mbena alisema dhana ya Usimamizi Shirikishi wa Misitu (USM) ni ya kuungwa mkono na viongozi ambao vijiji vyao vina misitu hasa ya miombo.

Mbena alisema vijiji vitano ambavyo vipo kwenye mradi wa TTCS umefanikiwa kuleta mageuzi hivyo wao wanawajibu wa kuunga mkono na kuendeleza.

"Mimi nitapambana kuhakikisha mradi huo unaendelea lakini pia naomba tupambane vijiji vipimwe kwani vila kuingia katika mpango wa matumizi bora ya ardhi hatuwezi kufanikiwa," alisema.

Diwani wa Konde, Clara Laurence  alisema vijiji vya kata yake havina misitu ya miombo ila vinaweza kutumia mfumo huo katika uvunaji wa mbao na kuwa na matokeo chanya.

"Kule kwangu miombo haipo lakini misitu ipo nadhani mfumo huu unapaswa kupelekwa ili kutumika katika uvunaji wa mazao mengine," alisema.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Kibena Kingo alisema katika kuonesha wamedhamiria kuendeleza halmashauri imekubaliana kutumia Msitu wa Sesenga Lumbachini kuanza mradi kama huo.

Kingo alisema ili kufanikisha dhamira hiyo ni jukumu la madiwani kushikamana kwa kuhakikisha fedha zinatengwa na kutumika eneo husika.

Wakuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili, Wahida Beleko, Asenga Christopher Ofisa Misitu, Idd Ndabhona Mwanasheria na wengine walisema wapo tayari kushirikiana na madiwani kuendeleza miradi ya USM vijijini

No comments:

Post a Comment

Pages