July 11, 2019

SAKATA KODI YA PANGO LA ARDHI LAANGUKIA MGODI WA GGML GEITA

 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiagana na Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) Richard Jordison alipotembelea mgodi huo kufuatilia ulipaji kodi ya pango la ardhi  mkoa wa Geita tarehe 10 Julai 2019.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza katika kikao baina yake na uongozi wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita uliopo mkoani Geita katika ziara yake ya kufuatilia ulipaji kodi ya pango la ardhi katika taasisi na makampuni mbalimbali yanayodaiwa kodi hiyo tarehe 10 Julai 2019. Kushoto kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa wilaya ya Geita Josephat Maganga na kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) Richard Jordison. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI). 

Na Munir Shemweta, WANNM GEITA

Operesheni maalum inayofanywa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula kupita ofisi moja hadi nyingine kuzibana taasisi na Makampuni yanayodaiwa kodi ya pango la ardhi imeangukia Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) uliopo mkoani Geita ambapo imebainika mgodi huo hauna hati miliki ya eneo hilo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 196.27 sawa na takriban hekta 19,927 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000 na hivyo kushindwa kulipa kodi ya pango la ardhi.
Akiwa katika ziara yake ya siku moja mkoani Geita tarehe 10, Julai 2019, Dkt Mabula alitembelea Mgodi huo wa Dhahabu wa Geita kwa lengo la kufuatilia ulipaji kodi ya pango la ardhi sambamba na kuangalia iwapo mgodi huo una hati miliki ya ardhi katika eneo hilo.
Hata hivyo, Dkt Mabula alielezwa na Mshauri wa Masuala ya Sheria ya Mgodi huo Elizaberth Karua kuwa GGML imekuwa ikilipa kodi mbalimbali serikalini lakini haijawahi kulipa kodi ya pango la ardhi kwa kuwa ina Leseni Maalum ya Uchimbaji Madini.
Kwa mujibu wa Karua, Mgodi wa Dhahabu wa Geita ambao uko ndani ya kampuni ya AngloGold Ashanti ya Afrika Kusini katika kipindi chote cha shughuli zake haujawahi kupewa wito wa kutakiwa kulipa kodi ya pango la ardhi na umekuwa ukizingatia Mkataba wa Uendelezaji Uchimbaji Madini (Mining Development Agreement).
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Denis Masami alieleza kuwa, kodi ya pango la ardhi inapaswa kulipwa na haina uhusiano wowote na leseni za uchimbaji madini kwa kuwa mmiliki wake anakuwa kama amepangishwa eneo na sheria ya Tanzania imetamka bayana kuwa ardhi itakuwa chini ya Raisi na kusisitiza kuwa kodi ya pango la ardhi inalipwa kama zinavyolipwa ankara za umeme na maji.
Kwa mujibu wa Masami, cha muhimu katika suala la kodi ya pango la ardhi ni umilikishwaji ambapo Mgodi wa Dhahabu wa Geita unatakiwa kutambulika kwa kuwa na nyaraka sahihi za umiliki na kusisitiza tafsiri ya sheria ya madini siyo sehemu ya ardhi.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Mabula pamoja na kuipongeza GGML kwa kuwa mlipaji mzuri wa kodi ya Serikali lakini eneo la Mgodi huo linapaswa kipimwa kutokana na kuwa katika mipango miji na sheria yake inaelekeza maeneo yote ya mipango miji kipimwa na kupangiwa matumizi.
‘’Eneo la Mgodi GGML lazima lipimwe na kupangwa kwa kuwa ndani ya mgodi kuna maeneo ya makazi, ofisi na matumizi mengine na vyote hivyo lazima vioneshwe katika ramani’’alisema Dkt Mabula.
Kwa mujibu wa Dkt Mabula, upimaji katika Mgodi huo wa GGML una faida kubwa kwa kuwa utaondoa migogoro ya ardhi ambayo baadhi yake husababishwa na wananchi kuingia maeneo ya mgodi na kutolea mfano Mgodi wa Nyamongo uliopo Tarime mkoa wa Mara baada ya kupimwa umeepusha migogoro iliyokuwa ikitokea sambamba na kulipa kodi ya pango la ardhi na kuutaka mgodi wa GGML kueleza ni lini utakuja na majibu wa kutaka kupimwa eneo lake.
Mshauri wa Masuala ya Sheria wa GGML Elizaberth Karua aliomba Mgodi huo kupewa muda wa wiki mbili kushauriana na uongozi wa juu kuhusiana na suala hilo kwa kuwa ujio wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ulikuwa wa kushtukiza ambapo Dkt Mabula aliupa Mgodi huo hadi tarehe 29 Julai 2019 kuja na majibu kuhusiana na suala hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita Richard Jordison alieleza kuwa ofisi yake iko tayari kushirikiana na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhakikisha suala hilo linafikia muafaka ili kuondoa migogoro.
Taarifa ya idara ya ardhi katika halmashauri ya Mji wa Geita inaeleza kuwa eneo la mgodi wa GGML halijapimwa bali lina alama za eneo lenye leseni ya uchimbaji ambazo hazina rekodi za upimaji na hivyo kuleta ugumu katika kuhakiki maeneo.

No comments:

Post a Comment

Pages