July 11, 2019

RT yatoa onyo kwa wanaovunja taratibu, ushiriki na uandaaji Marathons nchini

SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT), limeanza kuchukua hatua kwa wale ambao hawataki kufuata taratibu, kanuni na sheria katika uandaaji na ushiriki wa mbio mbalimbali za marathon nchini.

Kwa muda mrefu baadhi ya waandaaji wa mbio hizo na washiriki kutoka nje ya nchi, wamekuwa kwa makusuidi wakivunja taratibu kwa maslahi binafsi, bila kujali maslahi mapana ya maendeleo ya mchezo wa riadha hapa nchini.

Mfano wa watu hao ni waandaaji wa Kimondo Marathon iliyofanyika hivi karibuni mkoani Songwe, ambayo iliendeshwa kinyume cha sheria, taratibu na kanuni za RT pamoja na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

Pamoja na jitihada za RT kutuma mjumbe wa Kamati ya Ufundi (Lwiza John), ili kuwafahamisha waandaaji kwamba wanariadha wa nje ya nchi hawaruhusiwi kukimbia bila ruhusa ya Vyama vya Riadha vya nchi zao, lakini mjumbe wetu alipuuzwa na waandaaji pamoja na wanariadha hao watatu waliotoka nje ya nchi.

Kwa tafsiri rahisi ni kwamba, ubabe ulitumika kwa kisingizio cha mkuu wa mkoa "kashasema". Je mkuu huyo wa Mkoa ni wa Songwe ama wa wapi?

Pia tunafahamu kwamba, tuna tatizo kubwa la Mawakala ambao wanawaleta wanariadha wa nje ili wapate 15% ya fedha wanazoshinda, tutalipeleka sala hili BMT na kwa Waziri mwenye dhamana ya Michezo.

"Waandaaji wa Marathons wanapaswa kuwa wazalendo kwa kufuata sheria za RT ambazo pia ni za Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF), pia wathamini fedha wanazopata kwa wadhamini ambao ni kampuni na taasisi za kitanzania, zisiende nje ya nchi yetu kiholela sababu hizi ni kodi zetu,". 

Kimondo Marathon imeanzishwa kwa nia njema, lakini walikuwa na masilahi gani na wanariadha wa Kenya ambao hawakuwa na ruhusa?

Wakati RT ikiendelea na hatua zaidi kwa walioshiriki hujuma hizi Kimondo Marathon, Wanariadha watatu kutoka Kenya,  Denis Kemboi, Limo Peter na Karbolo Tatiyia walioshiriki bila ruhusa, hawataruhusiwa kushiriki mbio zozote za Tanzania hadi tutakapojadiliana kwa kina na Shirikisho la Riadha la Kenya (Athletics Kenya).

Tayari tumewaandikia AK na wameonyesha nia njema ya majadiliano, tunapenda kuwasisitiza waandaaji wote wa Marathons nchini, kufuata sheria na taratibu na RT itawapa ushirikiano wa kutosha.

No comments:

Post a Comment

Pages