July 22, 2019

WATOTO WA KIKE MSIKUBALI KUDANGANYWA – WAZIRI MKUU

*Awaonya vijana, wazee wanaotaka kuwaoa, asema miaka 30 jela ni yao
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.


Na Mwandishi Wetu
 
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watoto wa kike wasikubali kudanganywa na wanaume na badala yake wakazanie masomo hadi wahitimu elimu ya juu.

“Wasichana wote mliopo hapa, mwanaume yeyote akikufuatafuata mwambie usinusumbue; mwambie niache nisome. Kamwe msikubali kudanganyika, someni hadi mmalize Chuo Kikuu,” alisema. 

Ametoa wito huo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wakazi wa wilaya za Same na Mwanga akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za maendeleo mkoani Kilimanjaro. 

Waziri Mkuu ambaye alikuwa na ziara ya siku nne mkoani humo, amewaonya vijana na wazee ambao wana tabia ya kuweka mahusiano ya kimapenzi na watoto wa kike kwamba waache mara moja la sivyo wataishia jela. 

“Wanaume msisahau kwamba mtoto wa mwenzio ni wako. Nataka niwakumbushe kuwa ukimuona mtoto wa kike, muache. Huyo ni moto wa kuotea mbali. Ukimchumbia, ukimuoa, au kumpa mimba mtoto wa kike, ujue kuwa miaka 30 jela ni yako.”

“Serikali ya awamu ya tano, imeamua kuwekeza kwa mtoto wa kike, kwa hiyo tunataka watoto wa kike wakianza shule ya awali, wasome shule ya msingi, waende sekondari hadi wamalize Chuo Kikuu,” alisisitiza. 

No comments:

Post a Comment

Pages