July 19, 2019

WAZIRI MKUU AWAFUNDA WATUMISHI WA UMMA

*Ataka wawe na mipango kazi, asema Serikali inapima matokeo
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiongea na Viongozi na Watumishi wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, katika ukumbi wa Halmashauri Julai 19.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).   
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akikagua darasa lililokarabatiwa la Shule Kongwe ya Same Sekondari, mkoani Kilimanjaro Julai 19.2019. Kulia ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Same Sekondari Hoza Mgonja.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akikagua maabara katika Shule Kongwe ya Same Sekondari, kabla ya kuzindua mradi wa ukarabati wa shule hiyo kongwe, mkoani Kilimanjaro Julai 19.2019.         
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiangalia darasa lililokarabatiwa la Shule Kongwe ya Same Sekondari, katika mradi wa ukarabati wa shule hiyo kongwe mkoani Kilimanjaro, Julai 19.2019. 
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiangalia vitabu katika maktaba iliyokarabatiwa ya Shule Kongwe ya Same Sekondari, katika mradi wa ukarabati wa shule hiyo kongwe mkoani Kilimanjaro, Julai 19.2019. Kushoto ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Same Sekondari Hoza Mgonja.
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizindua mradi wa ukarabati wa shule kongwe ya Same Sekondari, iliyoko wilayani Same katika mkoa wa Kilimanjaro, Julai 19.2019. 
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na wanafunzi wa Same Sekondari mara baada ya kuzindua mradi wa ukarabati wa shule hiyo kongwe, iliyoko wilayani Same katika mkoa wa Kilimanjaro, Julai 19.2019.
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akimsikiliza mwanafunzi wa Same Sekondari, Omari Pundugu, akielezea changamoto mafanikio na changamoto za shule hiyo mara baada ya uzinduzi wa mradi wa ukarabati wa shule hiyo kongwe, iliyoko wilayani Same katika mkoa wa Kilimanjaro, Julai 19.2019.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwasalimia wananchi, baada ya kuzindua mradi wa ukarabati wa shule kongwe ya Same Sekondari, mkoani Kilimanjaro Julai 19.2019.

  

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa umma wawe na mipango ya kazi ambayo itaweza kupimika na kutoa matokeo.

“Kila mtumishi anapaswa awe na mpango kazi katika sekta yake na ni lazima aende kupima matokeo. Awamu hii, tunataka kuona matokeo ya kazi zenu." 

Ametoa kauli hiyo leo asubuhi (Ijumaa, Julai 19, 2019) wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Same kwenye ukumbi wa Halmashauri ya wilaya hiyo, mjini Same. 

“Watumishi mmeletwa kwenye wilaya hii ili muwahudumie wananchi. Tulioajiriwa, kazi yetu kubwa ni kuwatumikia wananchi bila ubaguzi wowote uwe ni wa kabila, itikadi au rangi.” 

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwakumbusha watumishi hao kwamba baada ya mchujo wa watumishi hewa, waliobakia wanapaswa kufanya kazi kwa bidii. 

"Fanyeni kazi kwa bidii, msimamo wa Serikali hii ni kwamba hatumvumilii mtumishi ambaye si mwajibikaji, ni mwizi, mzembe au anaomba rushwa. Serikali hii hatuna muda wa kujadili matatizo ya watumishi, tunamalizana hapo hapo," amesema. 

Amewataka watumishi hao wasimamie utekelezaji wa ahadi zilizotolewa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kwa sababu ndiyo chama tawala. 

"Mtumishi angalia sekta yako inasema nini, ifanyie kazi. Kama ni maji, tafuta ni wapi yanapatikana, changanua zinahitajika shilingi ngapi, tafuta njia ya kupata hizo fedha ili wananchi wapate maji." 

Kuhusu tabia ya kukaa ofisini, Waziri Mkuu amekemea tabia hiyo na kuwataka watumishi wote nchini waache tabia ya kukaa ofisini na badala yake waende vijijini kuwasikiliza wananchi. 

"Watumishi wa umma msikae ofisini. Nendeni vijijini walau kwa siku nne za juma. Hizo mbili zinazobakia, zitumieni kuandaa taarifa. Nendeni huko ili wananchi wasipate usumbufu wa kuja hapa mjini kuwatafuta," amesisitiza. 

"Mkuu wa Wilaya simamia zoezi la wakuu wa idara na wasaidizi wao kwenda vijijini. Wakienda vijijini ni lazima waonane na waheshimiwa madiwani, washirikiane kusikiliza kero na kutafuta majibu kwa wananchi. Huo ndiyo mshikamano wenyewe unaohitajika," amesema. 

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma watambue mipaka yao na wajenge mahusiano baina yao na wengine. 

Alitoa kauli hiyo jana jioni (Alhamisi, Julai 18, 2019) wakati akizungumza na watumishi wa Manispaa ya Moshi, kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. 

"Kila mmoja lazima atambue mipaka yake na mamlaka baina yake na wengine. Hapa mko wateuliwa, waajiriwa na wachaguliwa. Kila mtu ana nafasi yake ya kuwatumikia wananchi.

Aliwataka watumishi hao watambue falsafa ya Kiongozi mkuu wa nchi ambayo inahimiza uchapakazi. “Kwa hiyo tunaposema Hapa Kazi Tu, maana yake chapa kazi na tuone matokeo. Tunasisitiza kazi na tunataka kazi unayoifanya, itoe matokeo,” alisema. 

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,        
IJUMAA, JULAI 19, 2019.

No comments:

Post a Comment

Pages