August 05, 2019

DKT. MWANJELWA AWATAKA WANUFAIKA WA TASAF WENYE NGUVU WAFANYE KAZI BADALA YA KUSUBIRI RUZUKU

Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) amewataka wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambao wana nguvu za kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo wafanye hivyo, ili waweze kujiingizia kipato badala ya kutegemea ruzuku kutoka Serikalini kupitia TASAF.
Dkt. Mwanjelwa ametoa maagizo hayo alipokuwa akizungumza na wananchi na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika vijiji vya Lukindo na Burugo, Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Mkoani Kagera.              
                                
Dkt. Mwanjelwa amesema utawekwa utaratibu maalum ambao kila mwananchi mwenye uwezo wa kufanya kazi ambaye yuko kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini afanye hivyo na kulipwa ujira kutokana na kazi atakayoifanya. 
“Ni wajibu wa walengwa wote wenye uwezo wa kufanya kazi ambao wako kwenye mpango huu, wafanye kazi badala ya kutegemea ruzuku ili nguvu kazi yao isipotee bure,” Dkt. Mwanjelwa amesisitiza.  
  
Ameongeza kuwa, kufanya kazi kwa wanufaika hao ni sehemu ya kuwasaidia katika kuboresha maisha yao na kusisitiza kuwa ruzuku itabaki tu kwa wananchi wasioweza kufanya kazi ambao wengi wao ni wazee na watoto.
Aidha Naibu Waziri huyo amewataka wataalam wa halmashauri za wilaya nchini kote kuhakikisha kuwa wanafanya ufuatiliaji wa karibu kwa wanufaika ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi na tija kubwa.
Dkt. Mwanjelwa anaendelea na ziara ya kikazi mkoani Kagera kukagua utekelezaji wa shughuli za TASAF na kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma katika Halmashauri zote za mkoa huo ambapo tayari ameshatembelea Manispaa ya Bukoba na Halmashauri ya Bukoba Vijijini.
 Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akilakiwa na wananchi wa kijiji cha Burugo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Mkoani Kagera ambako yuko kwenye ziara ya kikazi kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF na kukutana na Watumishi wa Umma kuhimiza uwajibikaji.
 Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na wananchi  na Wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini  katika kijiji cha Burugo (hawapo pichani) juu ya utekelezaji wa miradi ya TASAF.
 Baadhi ya Wananchi na Wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika katika kijiji cha Lukindo kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Mkoani Kagera wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (hayupo pichani).
 Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (katikati) akiwa nyumbani kwa mmoja wa walengwa wa TASAF katika kijiji cha Burugo Bi. Justa Migini (kulia kwa Naibu Waziri) ni Meneja wa Miradi ya Ajira za Muda TASAF Bw. Paul Kijazi  wakishuhudia nyumba iliyojengwa na mlengwa huyo kwa kutumia ruzuku ya TASAF.
 Mmoja wa Wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa  kijiji cha  Burugo, Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Mkoani Kagera Bi. Agnes Kemilembe akitoa ushuhuda wa namna alivyotumia ruzuku kuboresha makazi yake kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb). Picha ya chini ni mlengwa huyo akimuonesha naibu waziri shamba lake analoliendeleza kwa kutumia ruzuku ya TASAF.

No comments:

Post a Comment

Pages