August 05, 2019

Puma kutoa gawiwo la shilingi bilioni 22

Meneja Sheria na Uhusiano wa Kampuni ya Mafuta ya Puma Tanzania, Godluck Shirima, akitoa maelezo kwa waandishi wa habari kuelezea ushirikiano wao katika Maonesho ya Nne Wiki ya Viwanda ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), yanafanyika jijini Dar es Salaam. (Picha na Suleiman Msuya).

NA SULEIMAN MSUYA

KAMPUNI ya Mafuta ya Puma Tanzania imesema katika mwaka 2018/2019 itatoa gawiwo la shilingi milioni 22 kwa wanahisa wake.

Aidha, kampuni hiyo imetoa shilingi milioni 300 kufadhili Mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ulionza jana jijini Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa na Meneja Sheria na Uhusiano ya Kampuni, Godluck Shirima wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya Rais John Magufuli kutembelea banda la Puma lililopo katika maonesho ya. Nne ya Wiki ya Viwanda ya SADC yanayofanyika jijini Dar es Salaam.

Shirima alisema Kampuni ya Puma imekuwa ikifanya vizuri mwaka hadi mwaka hivyo kuamua kuendelea kutoa gawiwo kwa wanahisa baada ya kuondoa gharama za usimamizi na miradi ya kijamii.

Meneja huyo alisema katika gawiwo hilo la shilingi bilioni 22 Serikali ambayo ina asilimia 50 ya Hisa itapata shilingi bilioni 11 na Puma bilioni 11.

Alisema kiasi hicho ni cha gawiwo ni ongezeko la bilioni 2 za mwaka 2017/2018 kwa kila mwana hisa ambapo gawiwo lilikuwa shilingi bilioni 18.

"Tunamuomba Rais atupe nafasi ili tuende kumkabidhi wenyewe gawiwo la shilingi bilioni 11 ambalo tunapaswa kuipata Serikali naamini mwakani litaongezeka," alisema.

Aidha, Shirima alisema ongezeko la gawiwo hilo linatokana mazingira mazuri ya kibiashara na uwepo wa miradi mikubwa yenye tija kwa nchi.

Alisema Puma imeweka mfumo wa mafuta katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na kutoa mafuta ujenzi wa Daraja la Salendar hivyo matumaini yao ni kupitia miradi hiyo mikubwa wataongeza gawiwo.

Kuhusu ufadhili wa mkutano wa SADC, Shirima alisema Kampuni ya Puma inafanya kazi na nchi 13 wanachama hivyo imeona irudishe fadhila kwa kuwa wadhamini wakuu.

Shirima alisema Kampuni ya Puma itaendelea kushirikiana na nchi wanachama wa SADC ili kuhakikisha dhamira ya nchi hizo kufikia uchumi wa viwanda inatimia.

Awali Rais Magufuli akitembelea mabanda aliipongeza kampuni hiyo kwa kazi nzuri wanayofanya na kusisitiza ushirikiano baina yao na Serikali.

No comments:

Post a Comment

Pages