August 06, 2019

KAMPUNI YA IMPALA GROUP YAKANUSHA KUFILISIKA KISA KUSHINDWA KULIPA MISHAHARA YA WAFANYAKAZI WAKE

Na Ahmed Mahmoud, Arusha

Uongozi wa hotel ya Impala na Naura hatimaye umelipa mishahara ya miezi miwili kwa wafanyakazi wake zaidi ya 257 waliokuwa wakidai na hivyo kuondoa Malalamiko yaliyojitokeza.

Uongozi wa Impala umesikitishwa na taarifa zilizoandikwa kupitia mitandao ya kijamii kuwa hotel hiyo imefilisika na kushindwa kujiendesha ikiwemo kulipa mishahara ya wafanyakazi wake na kudai kuwa jambo hilo si kweli kwa kuwa limelenga kuwachafua kibiashara.

Mkurugenzi wa hotel ya Impala na Naura ,Randy Mrema alisema wakati akiongea na vyombo vya habari mapema Leo  kuwa ,hotel zao bado zipo imara na kuwataka Wateja kutokuwa na hofu juu ya changamoto ndogo za mishahara ya wafanyakazi zilizojitokeza kwani jambo hilo ni mpito na limemalizika.

Alisema hotel za Impala na Naura ni hotel za Kitalii zenye uwezo wa kuwahudumia wageni wa aina mbalimbali duniani na wataendelea kushirikiana na serikali katika kuhakikisha wanakuza sekta ya utalii nchini kupitia hotel zao.

"Unajua tumeshtushwa sana na taarifa ambazo zimekuwa zikienea kwenye mitandao ya kijamii kwamba impala group imefilisika tunaomba wanaoeneza waje kwetu kupata taarifa sahihi na si vinginevyo" alisema Mrema

Alisema suala la wafanyakazi kutolipwa mishahara limekuwa likikuzwa na watu wenye nia mbaya kibiashara ili hotel hizo zionekane kuwa hazifai jambo ambalo si kweli.

Mkurugenzi huyo amewaomba wafanyakazi wake kuendelea na mshikamano wao wa siku zote tokea awali ili kuendeleza sekta ya Hotel za kitalii nchini na kuondoa malalamiko yasiyokuwa na tija ambayo yanaharibu mahusiano mazuri baina ya uongozi na wafanyakazi.

Alieleza kuwa impala group inategemewa na wakulima zaidi ya mia tano wanaokuja kuuza mazao yao ya mboga mboga na matunda wakiwemo pia wafugaji ambao wamekuwa wakiiuzia kampuni yetu na kujipatia kipato hivyo haoni sababu ya wao kushindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi hao.

Aidha alisema kuwa baadhi ya watoa huduma za  taxi na bodaboda waliopembeni ya hotel hizo wamestushwa na kusikitishwa na taarifa za hotel hizo kufilisika ambapo jambo hilo sio kweli na limeharibu taswira ya  kibiashara ya hotel hizo zilizo chini ya Impala group.

Alisema kuwa kimsingi hakuna jambo kama hilo la kufilisika na kuwataka wale wanaoharibu taswira nzuri ya impala group kuacha kufanya hivyo na tetesi kama hizo sio nzuri kibiashara.

Awali Mkurugenzi huyo pamoja na msaidizi wake Joram walidaiwa kuwekwa mahabusu kwa saa 24 kwa amri ya Mkuu wa wilaya ya Arusha Fabian Daqarro baada ya kushindwa kulipa wafanyakazi mishahara  yao jambo ambalo wanasema walishawalipa mishahara yao.

No comments:

Post a Comment

Pages