August 06, 2019

UJENZI WA BANDARI YA DAR ES SALAAM WAENDELEA VYEMA


Maendeleo ya ujenzi wa Bandari ya Dar es Salaam yanakwenda vizuri ambapo ujenzi wa magati 2 kati ya 7 yaliyopo umekamilika na kuanza kupokea meli kubwa za mizigo.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Mhandisi Deusdedit Kakoko amesema mradi wa ujenzi wa magati hayo utakaogharimu takribani shilingi Trilioni moja utaiwezesha Bandari ya Dar es Salaam kuongeza ufanisi kwa kuongeza kasi ya upakuaji na upakiaji wa mizigo na kupokea meli yoyote duniani zikiwemo meli kubwa za kizazi cha saba (7th Generation).

Mhandisi Kakoko amefafanua kuwa kazi inayoendelea imewezesha kukamilika kwa ujenzi katika gati namba 1 na gati namba 2 ambazo zimeongezwa kina kutoka mita 8 hadi kufikia kati ya mita 15 na 19, kina ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na kina kinahitajika kwa meli kubwa zaidi ambacho ni mita 12.

Aidha, Mhandisi Kakoko amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutilia mkazo ujenzi wa Bandari ya Dar es Salaam na kuamua kujenga gati nyingine ya magari iitwayo RORO ambayo itaiwezesha bandari hiyo kupokea meli hata 2 kwa mpigo zenyewe uwezo wa kuchukua magari 10,000 ikilinganishwa na uwezo wa kuchukua magari 200 kabla ya mradi huo.

“Sasa maana yake nini, magari ni kati ya shehena inayoingiza tozo zaidi, kwa magari pekee yake tunaweza kukusanya tozo mara 2 au mara 3 ikilinganishwa na kipindi cha nyuma, ndio maana tunamshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutuongezea hiyo gati ya RORO.

Kwa hiyo faida ya kwanza tunaipata katika kuongeza kina kwa maana meli kubwa zitaingia kwa mara moja, na kuna watu wamekuwa wakiona kuna Kijiji cha meli zinazosubiri kuingia bandari kushusha mizigo, hiyo haiwezi kuwepo tena” amesema Mhandisi Kakoko.

Mhandisi Kakoko amesema juhudi hizo zinakwenda sambamba na uboreshaji eneo la nyaraka (clearing) kupitia serikali mtandao ili kuondoa mianya ya udanganyifu ambao husababisha upotevu wa mapato.

“Sasa tutaweza kupata moja kwa moja Bill of Lading na hivyo kuondokana na baadhi ya wafanyabiashara au waagizaji mizigo ambao hudai makontena yana mitumba wakati ndani mna magari” amesema Mhandisi Kakoko na kubainisha kuwa uwekaji wa mfumo wa nyaraka unakwenda sambamba na uwekaji wa mitambo ya ukaguzi (scanner).

Amesema baada ya kukamilika kwa gati namba 1 na gati namba 2, ujenzi kwa sasa unaendelea katika gati namba 4 ambayo inakaribia kukabidhiwa TPA na gati namba 5 ambayo uchorongaji unaendelea.

Ameongeza kuwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa gati namba 3 na gati namba 4, ujenzi huo utaendelea kwa gati namba 5,6 na 7 na baada ya hapo kazi itaendelea kwa magati ambayo yapo chini ya Kampuni ya Kimataifa ya Huduma za Makontena Bandarini (TICTS) ambayo tayari Serikali ya Awamu ya Tano imeshafanya mazungumzo ya kurekebisha mkataba na sasa mrabaha unaolipwa ni mara 2 ikilinganishwa na zamani.

Mhandisi Kakoko amesema pamoja na kujenga gati hizo, Serikali pia inanunua mitambo mikubwa ya kupakulia na kupakia mizigo na hivyo kuongeza kasi na ufanisi zaidi wa bandari.

Kufuatia juhudi hizo amesema sasa bandari ya Dar es Salaam itakuwa na uwezo wa kutumia vizuri faida yake ya kijiografia kukabiliana na ushindani wa bandari zote zilizopo katika ukanda wa bandari ya Hindi na kuwa lango bora na muhimu kwa nchi za Afrika.

Mhandisi Kakoko amesema kazi hii ya uboreshaji wa Bandari a Dar es Salaam iliyopaswa kufanyika miaka 30 iliyopita imesababisha Tanzania kupoteza kiasi kikubwa cha mapato na kwamba kutokana na uboreshaji huu na hatua ambazo Serikali ya Awamu ya Tano imechukua, TPA itaendelea kuongoza katika utoaji wa gawio.

Ameahidi kuwa mwaka huu TPA inatarajia kutoa gawio la kati ya shilingi Bilioni 150 na shilingi Bilioni 200 na kwamba miaka michache ijayo TPA kwa kushirikiana na wadau wengine wa bandari watakuwa na uwezo wa kuzalisha fedha za kugharamia bajeti nzima ya Serikali ambayo ni takribani shilingi Trilioni 30 kwa mwaka.

Halikadhalika Mhandisi Kakoko amesema kazi ya ujenzi wa bandari pia inaendelea katika Bandari ya Mtwara na ujenzi katika Bandari ya Tanga utaanza mwezi huu (Agosti 2019)

No comments:

Post a Comment

Pages