HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 15, 2019

Kiswahili chapendekezwa SADC

NA SULEIMAN MSUYA

BARAZA la Mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wamekubaliana mapendekezo 107 likiwemo  Lugha ya Kiswahili kutumika rasmi kwenye vikao vya Jumuiya hiyo yenye miaka 39.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa SADC ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi wakati akifunga mkutano wa siku mbili ulioanza Agosti 13 hadi 14 uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Prof.Kabudi alisema makubaliano yao yamejikita katika masuala kiuchumi, kijamii, kisiasa na maendeleo kwa wananchi na  nchi wanachama.

Alisema Lugha ya Kiswahili ndio imetumika kutoa mafunzo kwa wapigania Uhuru wa nchi nyingi wanachama wa SADC hivyo kukubalika kutumika ni mapinduzi mapya ya lugha hiyo.

"Nawashukuru sana mawaziri wa SADC kukubali kwa pamoja Lugha ya Kiswahili kutumika kwenye vikao na mikutano ya Jumuiya huu ni ujumbe mzuri kwa mwasisi wa SADC, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere," alisema.

Alisema kwa sasa SADC itakuwa na lugha nne rasmi za vikao na mikutano iwapo Marais watakubali pendekezo hilo hivyo kurahisisha mawasiliano ya wananchi wote wa nchi wanachama.

Alisema awali lugha zilizokuwa zinatumika kwenye vikao vya SADC, ni kiingereza, kifaransa na kireno hivyo Kiswahili kinakuwa cha nne.

Aidha, alisema katika kikao hicho wamejadiliana mambo mbalimbali ya kusukuma maendeleo ya nchi za SADC.

Waziri Kabudi alisema wamekubaliana kila nchi kuwekeza katika viwanda ili kurahisisha upatikanaji wa ajira kwa wananchi wa nchi zao.

Mwenyekiti huyo alisema suala lingine ni eneo huru la kibiashara kwa nchi wanachama ilo kuchochea ukuaji wa biashara na uchumi.

"Nchi zetu bado zina hali mbaya katika kila sekta hivyo tumekubaliana kuongeza kasi katika uanzishaji wa viwanda, kutumia maeneo ya biashara huru kama kichocheo cha ajira na uchumi wa watu wetu," alisema.

Kabudi alisema pia mawaziri hao wamekubaliana kuungana kupigania Zimbabwe iiondolewe vikwazo iliyowekewa kwani wanaoumia ni wananchi na watoto wasio na hatia.

No comments:

Post a Comment

Pages