August 02, 2019

NMB Kuwawezesha wakulima kulima kisasa, Yadhamini Maonesho Ya Kitaifa Ya Nanenane Kwa Milioni 30

Na Mwandishi Wetu

NMB Kuwawezesha wakulima kulima kisasa, Yadhamini Maonyesho Ya Kitaifa Ya Nanenane Kwa Milioni 30
BENKI ya NMB imesema kuwa itahakikisha inaendeleza jitihada zake kwa wakulima za kuwawezesha kadri wanavyohitaji kulingana na mazao yao ili kuifanya sekta ya kilimo nchini kubeba uchumi wa nchi.

Mbali na hilo benki hiyo imesema kuwa kwa muda mrefu imekuwa ikitangaza sekta ya wakulima na kuwasaidia wakulima kama ajenda yake kuu, kutokana na asilimia kubwa ya watanzania kutegemea sekta hiyo.

Hayo yamesemwa na Meneja wa benki hiyo Kanda ya Magharibi Sospeter Magesse wakati akikabidhi kiasi cha sh. Milioni 30 na tisheti 300 kwa katibu tawala wa Mkoa wa Simiyu Jumanne Sagini kama udhamini wa benki hiyo kwenye maonesho ya Sikukuu ya Wakulima (Nanenane) kitaifa yanayofanyikia Mkoani humo. 

Magesse alisema kuwa benki hiyo imekuwa haifanyi kazi ya kutunza fedha za wateja wake tu, bali hata kusaidia jamii katika nyanja mbalimbali za Kilimo, Ufugaji, Elimu, Afya na Biashara.

Alisema kuwa katika maonesho hayo benki ya NMB imejipanga kuhakikisha inatoa elimu kwa wakulima, wafugaji, jinsi ya kulima kisasa na kitaalamu ikiwa pamoja na kuwaeleza jinsi gani benki hiyo inaweza kushiriki kwenye kilimo kwa kuwapatia mikopo.

“Kwenye maonesho ya mwaka huu ambayo yatakuwa bora zaidi, ushiriki wetu kama benki utakuwa mkubwa zaidi, na umelenga kuwasaida wakulima, tutakuwa na bidhaa za wafugaji wa ng’ombe, na wakulima wa mazao ya pamba, tumbaku na kahawa lakini hata Matrekta tutakuwa nayo,” alisema Magesse.

Aliwataka wakulima kujitokeza kwa wingi katika maonesho hayo hasa kwenye banda la NMB ili waweze kupata elimu itakayowafanya walime kisasa kwa kutumia teknoloJia na kuzalisha kwa tija.

Akiongea mara baada ya kupokea mchango huo Katibu Tawala huyo ameishukuru benki hiyo kwa mchango wake, ambapo alisema utawezesha kuboresha zaidi eneo la Nyakabindi ambako sherehe hizo zinafanyikia.

Sagini ameeleza kuwa Benki ya NMB imekuwa mstari wa mbele kusaidia mambo mbalimbali katika mkoa wa Simiyu ikiwemo Elimu na Afya, huku akibainisha kuwa mchango huo utawezesha maonesho hayo kuwa bora zaidi.

“Kwa mchango huu NMB watakuwa kwenye wachangiaji wale wa pili kwa ukubwa, tunawashukuru sana kwa mchango wao na tuombe mahusiano yetu na wao yaendelee kuwa mazuri zaidi ya hapa,” alisema Sagini.
 Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu Jumanne Sagini (wa pili kulia) akipokea mfano wa hundi kutoka kwa Meneja wa NMB Kanda ya Magharibi Sospeter Magese. Fedha hizo zitatumika kwenye maonesho ya NaneNane ya kitaifa. NMB ni wadhamini wa Maonyesho hayo ya kitaifa yanayolenga kutoa fursa kwa wakulima na Wafugaji.
Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe (wa pili kushoto) akitazama bidhaa za mfanyabiashara Raphael Buja (Buja Pure Honey) kwenye Banda la NMB wakati wa uzinduzi wa maonesho ya Nanenane katika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu. Kushoto ni Meneja Mwandamizi Biashara na Kilimo wa NMB John Machunda na Mkuu wa Idara wa Biashara kwa Serikali NMB Vicky Bishubo.
Wananchi wakipata huduma mbalimbali kwenye banda la NMB, wakati wa uzinduzi wa maonesho ya Nanenane katika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu walipotembelea banda hilo. NMB ni mmoja wa wadhamini wakuu wa maonesho hayo.

No comments:

Post a Comment

Pages