HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 14, 2019

SADC YATAJA CHANGAMOTO ZINAZOKWAMISHA UTEKELEZAJI WA MIPANGO YAO

 Katibu Mkuu wa SADC, Dk. Stergomena Tax, akizungumza wakati wa uzinduzi wa machapisho matano yaliandaliwa na Kituo cha Utafiti na Machapisho Kusini mwa Afrika (SARDC).
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu (wa pili kulia), Katibu Mtendaji wa SADC Dk. Stergomena Tax (katikati) na  Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, Madaraka Nyerere (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Utafiti na Machapisho Kusini mwa Afrika SARDC, Munetsi Madakufamba,  wakizindua machapisho matano ya SADC yahusuyo Mkakati wa maendeleo ya amani na usalama, Mkakati wa ufuatiliaji masuala ya Jinsia, Mkakati na mpango wa kushughulikia ukatili wa Kijinsia, Mkakati wa Nishati na Mkakati wa tathmini fupi ya uendelezaji wa Miundombinu kwa kwa nchi za SADC, wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam.

NA SULEIMAN MSUYA

JUMUIYA ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imetaja changamoto mbili kubwa zinazokwamisha utekelezaji wa mipango yao kwa nchi wanachama.

Changamoto hizo zimetajwa na Katibu Mkuu wa SADC, Dk. Stergomena Tax, jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa machapisho matano yaliandaliwa na Kituo cha Utafiti na Machapisho Kusini mwa Afrika (SARDC).

Dk.Tax alisema SADC imekuwa ikiandaa mipango mingi mizuri kwa nchi wanachama lakini changamoto kubwa ni nchi kutekeleza ili kufikia malengo wanaojiwekea.

Alitaja changamoto hizo kuwa ni nchi wanachama kushindwa kuhuisha mipango ya SADC kwenye mipango ya kitaifa.

Alisema iwapo mipango haiwekwi kwenye mipango ya kitaifa ni vigumu utekelezaji kufanyika kwa wakati.

Katibu Mkuu hiyo alisema changamoto nyingine ni sekta binafsi kutoshiri kikamilifu kwenye ujenzi wa miundombinu.

Alisema kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa na SARDC kati ya mipango 134 ambayo SADC walikubaliana utekelezaji ni asilimia 5 tu hali ambayo inatoa picha mbaya ya kufikia uchumi wa viwanda.

Dk.Tax alisema machapisho hayo matano yameonesha namna gani nchi wanachama zinatekeleza makubaliano wanayofikia katika vikao vyao na nini cha kufanya.

Akizungumza machapisho hayo Mkurungezi Mkuu wa SARDC, Munetsi Madakufamba, alisema machapisho hayo yameweza kuonesha njia sahihi ya nchi wanachama wa SADC kufikia maendeleo jumuishi.

Madakufumba alisema chapisho la kwanza la mkakati wa SADC kuwajumuisha wanawake kwenye ulinzi na usalama limelenga kuwataka wanawake wanashiriki kila jambo kwa usawa.

Alisema kuhusu chapisho la pili linalozungumzia ufuatiliaji wa usawa wa kijinsia kwenye maendeleo alisema nchi nyingi za SADC bado zina hali mbaya.

"Katika eneo hili nchi ambazo zimefanya vizuri ni Afrika Kusini na Shelisheli ambapo uwakilishi upo 50/50 huku Tanzania ikifuata kwa asilimia 37," alisema.

Mkurugenzi huyo alitaja machapisho mengine kuwa ni SADC mkakati na mpango wa kushughulikia ukatili wa kijinsia, ufaatiliaji wa maendeleo ya nishati na mpango mfupi wa kutathmini maendeleo ya miundombinu.

Madakufamba alisema iwapo kutakuwa na uthubutu wa pamoja katika utekelezaji wa makubaliano ambayo nchi za SADC zinafikia ni dhahiri maendeleo yatapatikana kwa kasi.

Alisema iwapo nchi zote wanachama zitashirikiana kwa pamoja kwa kuweka mikakati yao kwa mipango ya taifa ni dhahiri mafanikio yataonekana.

Mjumbe wa Bodi ya SARDC, Madaraka Nyerere alisema kituo hicho kimejikita kufanya tafiti katika ukanda huo ili kuweza kusaidia sekretarieti ya SADC kufanya kazi zake za kuchochea maendeleo kwa usawa.

"Kituo hiki ni kisima cha maarifa kwa nchi za SADC hivyo kitukike kuchochea maendeleo ya ukanda huu ambao umekuwa pamoja kwa miaka 39 sasa," alisema.

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema Tanzania imekuwa ikitekeleza makubaliano ya SADC hatua kwa hatua.

Mwalimu alisema serikali imekuwa ikitekeleza makubaliano hayo kwa kutoa  mikopo kwa wakina mama ambapo zaidi shilingi bilioni 3 zimetolewa.

"Pia ongezeko la ushiriki wanawake kwenye vikao vya maamuzi limefanyika kutoka asilimia 22 mwaka 2010 hadi 37 kwa sasa. Lakini pia elimu bure imechochea watoto wakike kujiunga na elimu ya msingi na sekondari," alisema.

Kwa upande wake Waziri wa Nishati, Dk.Merdad Kalemani alisema Tanzania ipo kwenye mchakato wa kutekeleza miradi ya kikanda ya umeme kwa siku za karibuni.

Kalemani alitaja miradi hiyo kuwa ni uzalishaji Kilovoti 400 kutoka Iringa, Mbeya, Malawi na Zambia na mradi wa umeme Kilovoti 400 kutoka Singida, Zambia na Kenya.

Kuhusu dhana ya jinsia alisema Serikali inaendelea kusambaza umeme vijiji ambapo hadi sasa asilimia 60 ya vijiji ina huduma umeme hivyo kuwaondolea adhaa wanawake.

Alisema matarajio yao ni ifikapo 2021 vijiji vyote viwe na umeme na kwamba ujenzi wa Mradi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere (JNHPP), umekuja kutatua kero hiyo.

No comments:

Post a Comment

Pages