Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk. Angeline Mabula
akizungumza na wananchi wa eneo la Uledi kata ya Mpera katika Manispaa
ya Tabora wakati wa kukabidhi Hati za Ardhi akiwa katika ziara yake
mkoani Tabora leo. kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya
Magharibi Idrisa Kayera.
Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk. Angeline Mabula
akimkabidhi Hati ya Ardhi Jenita Mapunda katika eneo la Uledi Kata ya
Mpera Manispaa ya Tabora wakati wa ziara yake mkoani Tabora. (Picha na Wizara ya Ardhi).
Na Munir Shemweta, WANMM TABORA
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk. Angeline Mabula amekemea ucheleweshaji utoaji
Hati za Ardhi katika Manispaa ya Halmashauri ya Tabora mkoani Tabora na kueleza
kuwa hali hiyo inachangia kuikosesha serikali mapato yatokanayo na kodi ya
ardhi.
Dkt Mabula alitoa kauli
hiyo tarehe 13 Agosti 2019 wakati wa ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji
maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi pamoja na kukagua mifumo ya kodi kwa
njia ya kielektronik na Masijala ya ardhi katika mkoa wa Tabora.
Kauli ya Naibu Waziri
wa Ardhi inafuatia kubaini uwepo Hati za Ardhi 92 katika Manispaa hiyo ambazo
hazijafanyiwa kazi kwa muda mrefu kwa maelezo kuwa baadhi ya majalada ya hati
hizo yalikuwa na upungufu na wahusika wake hawapatikani.
Dkt Mabula alishangazwa
na hali hiyo kwa kuwa baadhi ya maombi ya Hati za Ardhi yana zaidi ya miaka
miwili katika Ofisi ya Afisa Ardhi Mteule wa Manispaa ya Tabora tangu mwaka
2016 bila kufanyiwa kazi jambo alilolieleza kuwa linawakatisha tamaa wananchi
wanaoomba Hati.
Kufuatia hali hiyo,
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alimuagiza
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora Bosco Ndunguru kumuandikia
barua ya onyo Afisa Ardhi Mteule wa Daudi Msengi kwa kushindwa kuwajibika
ipasavyo.
Kwa mujibu wa Dkt
Mabula, kwa sasa Wizara yake haitamvumilia Mtumishi yeyote wa sekta ya ardhi atakayeshindwa
kutekeleza majukumu yake na kusisitiza kuwa kuwa upandishwaji vyeo kwa watmushi utazingatia
utendaji kazi na kuwataka kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Amezitaka Halmashauri
nchini kupanga malengo ya uandaaji Hati za Ardhi kwa watendaji wake ili kuelewa
kwa siku moja zinaandaliwa Hati ngapi na kufafanua kuwa hiyo itazisaidia
halmashauri kufikia malengo ya utoaji hati. Dkt Mabula alitolea mfano wa
halmashauri ya Ilemela mkoani Mwanza kuwa imejiwekea malengo ya kuandaa hati
tano kwa siku moja jambo lililoiwezesha kuandaa hati nyingi na hivyo kuwa moja
ya halmashauri inayofanya vizuri kwa utoaji Hati za Ardhi.
Dkt Mabula alisema,
manispaa ya Tabora imeshindwa hata kutimiza malengo yake ya kutoa hati katika
mwaka wa fedha 2018/2019 ambapo Manispaa hiyo ilijiwekea kutoa jumla ya Hati 2000
lakini ilifanikiwa kutoa 1200 tu.
Aidha, alitaka suala la
kuandaa Hati za Ardhi lifanywe na Maafisa Ardhi kwa kuwa wote wana taaluma ya
ardhi badala ya kumtegemea Afisa Ardhi Mteule ambaye wakati mwingine amekuwa akichelewesha kwa kisingizio cha kutingwa
na shughuli nyingi.
Ameitaka Manispaa ya Tabora
kuongeza kasi ya utoaji Hati za Ardhi kwa wananchi katika Manispaa hiyo ili kuwamilikisha na
kuchangia mapato ya serikali kupitia kodi ya ardhi sambamba na kuhimiza Maafisa
Ardhi kuwa na kauli nzuri kwa wateja kwa
lengo la kujenga mazingira mazuri ya utendaji.
Katika
hatua nyingine Naibu Waziri wa Ardhi nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewakabidhi wananchi kumi na tano wa
eneo la Uledi katika Kata ya Mpera mkoani Tabora Hati za Ardhi kwa niaba ya
wenzao takriban 2117 baada ya kukamilisha taratibu za kupatiwa hati.
Dkt Mabula alisema
usalama wa miliki ya ardhi ni kupatiwa Hati ya Ardhi na kusisitiza usalama wa
eneo siyo kuwekewa Beacons pekee bali wananchi wanahitaji kupatiwa hati ili
ziweze kuwasaidia katika shughuli za uchumi ikiwemo kuchukua mikopo benki.
Ameagiza kukamatwa kwa
wale wote waliohujumu alama za mipaka katika maeneo ya ardhi eneo la Uledi kwa
kung’oa Beacons na kusisitiza kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria na wote
waliofanya kosa hilo wachukuliwe hatua ikiwemo kufikishwa katika vyombo vya
sheria
Kamishna Msaidizi wa
Ardhi Kanda ya Magharibi Idrisa Kayera alisema upimaji ardhi katika Manispaa ya
Tabora kwa sasa umeongezeka tofauti na miaka ya nyuma ambapo maeneo mengi
yanapimwa na kupangwa na kubainisha kuwa ofisi yake itahakikisha wananchi
wanamilikishwa na kueleza kila mwananchi mwenye eneo kufuatilia taratibu za
kumilikishwa.
No comments:
Post a Comment