August 04, 2019

WANANCHI WA KATA YA IRISYA MKOANI SINGIDA WAFURAHIA KUPATA MAJI YA BOMBA

 Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu, akihutubia  mkutano wa hadhara uliofanyika  Kata ya Irisya wilayani Ikungi mkoani Singida jana.
 Diwani wa Kata ya Irisya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ali Mwanga akizungumza.
 Mkutano ukiendelea.
Na Dotto Mwaibale, Singida

WANANCHI wa Kata ya Irisya iliyopo wilayani Ikungi mkoani Singida wamefurahia kupata maji ya bomba ambayo hawakuwahi kuyapata tangu nchi hii ipate  uhuru.

Kupatikana kwa maji hayo kumetokana na jitihada za Mbunge wao wa Jimbo la  Singida Magharibi, Elibariki Kingu za kuwaletea maendeleo katika jimbo hilo kwa kushirikiana na Serikali.

Akizungumza jana katika mkutano wa hadhara aliouandaa mbunge huyo Diwani wa Kata hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ali Mwanga alisema ilikuwa ni chereko na nderemo kwa wananchi wa Kata hiyo na vitongoji vya jirani baada ya kupata maji kwa mara ya kwanza kwenye kata hiyo.

Alisema juzi ilikuwa ndio siku ya kufanya majaribio ya kutoa maji baada ya kupelekewa mradi mkubwa wa maji na Serikali kupitia mbunge wao.

Alisema baada ya kufunguliwa maji hayo wananchi wa kata hiyo waliweza kuteka maji hayo kwa zaidi ya masaa matano huku wengine wakitoka umbali wa kilomita nne hadi tano jambo ambalo lilionesha furaha kwao.

Alisema kuwa bomba hilo lina uwezo wa kutoa maji lita 18,600 kwa saa ambapo ni sawa na pipa 740 na kuwa kata hiyo itajitosheleza kwa maji na ziada itakwenda vitongoji vingine vya jirani.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Kata hiyo, Juma Nkungu alisema tangu wamepata Uhuru hakuna mbunge ambaye aliwahi kuwafikia wananchi kwa kuwapelekea maendeleo kwa kiasi hicho kama Kingu.

"Kwa kusema ukweli Kingu amegusa kila kitongoji cha jimbo letu katika kuleta maendeleo tunasema hatumtaki mbunge mwingine zaidi yake kwanza anamsaidia sana Rais wetu Dkt.John Magufuli na tunamuhakikishia katika chaguzi zinazo kuja tutawapa kura za kutosha kuanzia  Rais, Mbunge na Diwani wetu Ali Mwanga" alisema Nkungu.

Akihutubia katika mkutano huo Kingu alisema katika kipindi cha miaka minne tangu wachaguliwe serikali ya awamu ya tano imefanya kazi kubwa ya maendeleo katika nchi hii baada ya Rais Dkt.John Magufuli kudhibiti fedha zilizokuwa zikitumika hovyo na kuziba mianya ya wizi na fedha hizo kuzielekeza katika shughuli za maendeleo kama vile ununuzi wa ndege, ujenzi wa vituo vya afya, barabara, umeme, reli na miradi mingine.

No comments:

Post a Comment

Pages