August 04, 2019

ZOEZI LA KUPIMA UTAYARI WA KUKABILI EBOLA LA ACHA ALAMA MKOANI KAGERA

Watumishi wa Afya wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa, Bukoba, mkoani Kagera,wakiendelea kufanya mazoezi ya namna ya kuvaa vifaa kinga kwa ajili ya kumhudumia mgonjwa anayehisiwa kuwa na maabukizi ya  ugonjwa wa Ebola,  katika hospitali hiyo Agosti 2019. (Picha na OWM).


Na OWM, KAGERA

Serikali kupitia uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Menejimenti ya Maafa kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, pamoja na wadau wa maendeleo,   imefanikiwa kufanya zoezi la kupima utayari wa kukabili ugonjwa wa Ebola katika mkoa wa Kagera katika wilaya tatu za mkoa huo kwa kuhusisha  watoa huduma za Afya katika wilaya hizo za  Bukoba, Misenyi na Ngara.

Zoezi hilo limefanikiwa kuwaimarisha watumishi hao katika maeneo maalum ikiwemo ya uratibu, utambuzi na ufuatiliaji wa wagonjwa iwapo wakipatina, matibabu ya wagonjwa, uchukuaji na usafirishaji wa sampuli na kuthibitisha maabukizi pamoja kuimarisha mifumo ya utambuzi wa masuala ya Afya kwa kila abiria wanaopita kwenye mipaka ya mkoa wa Kagera.

Akiongea kuhusu kuhitimishwa kwa zoezi hilo jana tarehe  3 Agosti, 2019, mkoani Kagera, Mkurugenzi Msaidizi (Utafiti na Mipango), Idara ya Menejimenti ya Maafa,   ofisi ya Waziri Mkuu, Bashiru Taratibu, ameeleza kuwa watumishi wa sekta ya Afya katika maeneo yote ambayo zoezi hilo limefanyika wameweza kuimarishwa katika suala la  uratibu hususani katika kuhakikisha kuwa rasilimali zote zinazohitajika pindi ikigundulika kuwepo kwa mgonjwa wa Ebola zinapatikana kwa wakati na kwa kutosheleza mahitaji pamoja na kutumika kwa usahihi.

Aidha, Mratibu wa zoezi hilo toka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, ambaye pia ni Mtaalamu wa Afya ya Jamii, Dharura na Maafa,  Dkt. Faraja Msemwa amefafanua kuwa timu ya  wataalamu wa sekta za Afya na Uratibu wa Shughuli za serikali, kutoka Wizarani, Idara na Mashirika ya Kimataifa,   wamefanikiwa kuendesha   zoezi hilo kwa watoa huduma wa Afya kwa wilaya tatu za mkoa huo hususan zilizopo  mipakani.

“Zoezi letu tumefanikiwa  kulihitimisha mkoani hapa tayari kwa kufanya zoezi la kupima utayari wa kukabili ugonjwa wa Ebola kwa watoa huduma wa Afya kwa vituo vya Afya vya  Nshambya, Kabyaile, Kabanga, Bunazi pamoja na Hospitali ya Rufaa ya mkoa ya Bukoba.Tunaamini kufanikiwa kufanya zoezi hili limeboresha utendeji wa watoa huduma hao katika kukabili ugonjwa wa Ebloa” alisema Dkt. Msemwa

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Marco Mbata amefafanua kuwa kufanyika kwa zoezi hilo mkoani humo kumewawezesha kujua maeneo gani ya kuboresha wakati wa ugonjwa wa Ebola na watumishi  wameelewa kwa vitendo wapo tayari kukabili ugonjwa huo.

“Tunashukuru vifaa tunavyo vya kutumia wakati wa kujikinga iwapo atatokea mgonjwa wa Ebola, hivyo kupitia zoezi hili tumeongeza uelewa wa kujikinga wenyewe, kuwakiknga watu walio karibu na mgonjwa pamoja na jamii nzima. Tumeweza kujifunza jinsi ya kumpokea mgonjwa, kuchukua vipimo hakika zoezi hili limetujenga  ” alisisitiza Mbata.

Naye Mratibu wa Vituo vya Mipakani, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Remedius Kakuru amebainisha kuwa kupitia zoezi hilo limeimarisha utendaji wa maafisa Afya wa mipakani kwa kuzingatia kuwa  tayari serikali imenunua vifaa vya kisasa muhimu vinavyo hitajika kwa ajili ya utambuzi wa abiria mwenye maambukizi ya ugonjwa wa Ebola ikiwemo Vipima  joto la mwili “themo scanners”.Vifaa hivyo  vyenye uwezo wa kupima joto la mwili la abiria wanao pita katika mipaka ya Tanzania vina uwezo wa kupima joto la mwili kwa kuwa ndiyo kiashiria  kikuu kimojawapo kwa mgonjwa mwenye maabukizi ya Ebola .

Kwa upande wake Afisa  anayeshughulika na Magonjwa ya Mlipuko kutoka Shirika la Afya Duniani, hapa nchini, Anthony Kazoka alieleza kuwa Shirika la Afya Duniani linaendelea kushirikiana na serikalai ya Tanzania katika kulinda Afya za watu wake kwa kutoa utaalamu katika zoezi hilo  kwa kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimo hatarini kupata mlipuko wa ugonjwa wa Ebola. Hivyo kwa kufanyika zoezi  hilo kwa mafanikio kutasaidia Tanzania kuwa salama na kuwa chanzo cha kuiweka Dunia salama kwa kutambua maabukizi ya ugonjwa huo mapema iwapo yatatokea.

Kufuatia nchi ya jirani (DRC) kuendelea kukabiliwa na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola tangu Agosti mwaka 2018. Tanzania imeendelea kuchukua tahadhari za ugonjwa huo kwa kupima utayari wa Watoa huduma za Afya kwa mikoa ya mipakani ukiwemo mkoa wa Kagera. Mkoa huo ambao unapakana na nchi ya Uganda ambayo  inapakana na DRC lakini pia  imekuwa na wagonjwa kadhaa wa Ebola.

Zoezi hilo linaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa ushirikiano na wadau wa maendeleo ambao ni WHO, FAO, USAID, HRH2030, na USAID Global Health Supply Chain Programu. Zoezi hilo limefanyika kwa muda wa wiki moja ambapo limekamilika tarehe 3 Agosti mwaka 2019, kwa kufanyika  katika vituo vya kutolea huduma za afya na maeneo ya mipaka ya  mkoani  wa Kagera.

No comments:

Post a Comment

Pages