Afisa Maendeleo ya Jamii
Halmashauri ya Mji wa Nzega Bi. Mwajuma Kisoma (kushoto) akikabidhi Kitini cha
Elimu ya Malezi kwa familia kwa Katibu wa Kikundi cha Malezi ya Happy Bi. Neema
Nogigwa (kulia) mara baada ya mafunzo ya elimu ya familia kwa kikundi cha malezi cha Happy.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WAMJW)
Na Mwandishi Wetu Nzega
Imeelezwa kuwa uanzishwaji wa vikundi vya malezi kwa familia itasidia kwa kiasi kikubwa kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika familia hasa kwa watoto vinavyoendelea kushamiri kila kukicha.
Hayo yamebainika wakati watalaamu kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii walipokuwa wakitoa elimu ya malezi ya familia na kuratibu uanzishwaji wa vikundi vya malezi katika Kata mbili za Halmashauri ya Mji wa Nzega mkoani Tabora.
Akizungumza katika Kata ya Nzega Magharibi Mkurugenzi Msaidizi Familia kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Idara Kuu ya maendeleo ya Jamii Bi. Tausi Mwilima amesema kuwa mwaka 2015 Serikali ilikuja na Kitini cha malezi kwa familia kilicholenga kutoa elimu kwa Maafisa Maendeleo ya jamii kuanzia ngazi ya mkoa hadi Kata ili wakaitoe elimu hiyo kwa jamii na kuwezesha uanzishwaji wa vikundi vya malezi vitakavyosaidia mapambano ya kuondokana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika jamii.
Ameongeza kuwa lengo la kuanzishwa kwa vikundi vya malezi katika jamii ni kuisaidia jamii kupata elimu sahihi ya malezi ili kuondokana na vitendo vya kikatili.
Bi. Tausi amesema kuwa jamii inawajibu wa kuhakikisha kuwa watoto wanapata malezi bora ambayo yatamuweka mbali na vitendo vya ukatili ambapo kwa sehemu kubwa vimekuwa vikiwaharibu watoto hasa kisaikolojia.
Ameongeza kuwa Serikali katika kuhakikisha vikundi hivyo vinapata nguvu ya kutekeleza wajibu wao inaratibu utoaji wa Elimu ya Malezi ya Familia ambayo itawasaidia kuwapatia wazazi au walezi nyenzo muhimu za namna ya kuwapa malezi bora watoto katika jamii.
Bi. Tausi amesisitiza vikundi vya malezi kusimamia vizuri malezi bora kwa watoto na kuwezesha kuwa na taifa lenye kuwajibika katika kuwajenga watoto katika malezi.
"Vitendo vingi vya ukatili kwa watoto vinafanywa na wazazi/walezi na watu wa karibu hivyo tunahitaji elimu ya malezi ili kuhakikisha tunatokomeza vitendo hivi" alisema Bi. Tausi
Kwa upande wake Katibu wa kikundi cha malezi cha Happy kilichopo Kata ya Nzega Magharibi Bi. Neema Nogigwa amesema kuwa elimu ya malezi ya familia waliyoipata imewapa nguvu na ujasiri wa kuzifikia familia na kuzipata elimu hiyo na watoto walioathirika na vitendo vya ukatili.
Ameongeza kuwa wao kama kikundi cha malezi cha Happy wanaahidi kuzifikia jamii ambazo hazijapata elimu ya malezi ya familia ili kuzuia ukatili dhidi ya watoto nchini.
Naye mjumbe wa kikundi cha malezi cha Happy kilichopo Kata ya Nzega Magharibi Bi. Salvasia Kapalata amesema kuwa mafunzo ya elimu ya malezi waliyoyapata wataitoa kwa vikundi vingine katika maeneo yao ili kuisaidia jamii kuondokana na vitendo vya ukatili katika familia kwani mara nyingi familia zimekuwa zikifanya vitendo vya ukatili bila kujua kama wanawakatili watoto.
Wakati huo huo mjumbe wa kikundi cha Malezi cha Amani Kata ya Nzega Mashariki Shule ya Sekondari Nzega Bw. Ntobi Nzwili amesema kuwa mwanzo walikuwa wanatoa elimu lakini walikuwa hawana muongozo sahihi wa utoaji wa elimu ya malezi ila baada ya kupata elimu hiyo wataweza kuendelea kutoa elimu sahihi ya malezi kwa familia itakayowasaidia kuilinda jamii ili kuondokana na vitendo vya ukatili katika maeneo yao.
Naye Mjumbe wa Kikundi cha Malezi cha Amani Bi. Winfrida Nkugwe ameishukuru Wizara kwa kutoa elimu ya malezi kwa kikundi chao na amehaidi kuwa wataitoa elimu katika vikundi vingine vya jumuiya katika nyumba za ibada na mitaani ili kuelimisha jamii kuhusu malezi bora kwa familia.
No comments:
Post a Comment