RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete, jana
alinogesha vilivyo mbio za Brazuka Kibenki Marathon zilizofanyika viwanja vya
JMK Park, Kidongo Chekundu jijini Dar es Salaam.
Mbio hizo maalumu zilizoandaliwa na Benki 16 nchini, zilikuwa
na lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia watoto wenye matatizo ya
moyo katika Taasisi ya Jakaya Kikwete(JKCI).
Rais mstaafu Kikwete, alishiriki Mbio za Kilomita 5 na
kufanikiwa kumaliza, kuanzia viwanja vya JMK Park na kupita barabara mbalimbali
za Jiji la Dar es Salaam na kuishia kwenye viwanja hivyo.
Akizungumza mara baada ya kumaliza mbio hizo, JK alizipongeza
benki zilizofanikisha tukio hilo, sambamba na washiriki na kwamba anatarajia
tukio hilo litakuwa endelevu mwakani.
Kwa upande wa Kilomita 15 Wanaume, Elibariki Buko wa Lumumba,
alishinda akitumia dakika 48:17 akifuatiwa na Paul Masenza wa DRC dakika 49:12
huku nafasi ya tatu ikienda kwa Edson Mwakalukwa 49:55 kutoka Klabu ya DRR za
jijini Dar es Salaam.
Kilomita 15 wanawake, mshindi aliibuka Rose Malya kutoka
Klabu ya Runners aliyetumia dakika 60:07 akifuatiwa na Monica Lugendo wa Dar es
Salaam 61:00 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Beatrice Edward kutoka Gardaworld
ya jijini Dar es Salaam dakika 62:27.
Kwenye mbio za Kilomita 10 wanaume mshindi aliibuka Twaha
Ally aliyetumia dakika 32:20 akifuatiwa na Sulan Lwamba 32:29 na nafasi ya tatu
ikaenda kwa Masamaki Rashid dakika 33:40 wote kutoka Dar es Salaam.
Wanawake Kilomita 10, mshindi aliibuka Mia Mjengwa kutoka
Iringa dakika 36:40 akifuatiwa na Lilian Chiume wa Mbezi Beach 36:59 huku
nafasi ya tatu ikishikwa na Palina Nijne dakika 37:00.
Kilomita 5 Wanaume, nafasi ya kwanza ilikwenda kwa John
Silima aliyetumia dakika 15:17 akifuatiwa na Jeremiah Baruti 15:85 huku nafasi
ya tatu ikinyakuliwa na Joseph John 16:00 wote kutoka Mlimani Academy.
Wanawake Kilomita 5, mshindi aliibuka Hamisa Moshi wa Mlimani
Academy dakika 18:20, nafasi ya pili Anna Mushi 18:47 huku wa tatu akiwa ni Neema
Nsunza wote wa Dar es Salaam.
Pia kulikuwa na zawadi ya medali kwa watoto walioshiriki na
kufanya vizuri.
No comments:
Post a Comment