HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 14, 2019

Rais Magufuli atumia Bil.1.6/- kukarabati shule alizosoma Julius Nyerere

Rais John Magufuli akikagua dawati lililowekwa kama alama ya eneo alilopenda kukaa Mwalimu Nyerere akiwa anasoma Shule ya Mwisenge mkoani Mara.
 Bweni alilolala Mwalimu Nyerere katika Shule ya Mwisenge kabla ya ukarabati.
 Bweni alilolala Mwalimu Nyerere katika shule ya Mwisenge baada ya ukarabati.
Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Mwisenge B, Jones Lumbe, akizungumza na Wanahabari waliotembelea shule hiyo hivi karibuni.
 Sehemu ya mbele ya chumba maalum chenye kumbukumbu ya maandiko ya Mwalimu Nyerere na hostoria ya Safari ya Azimio la Arusha iliyohifadhiwa kwenye Shule ya Sekondari ya Tabora Wavulana.
 
 
Na Irene Mark

SERIKALI ya awamu ya tano, imetumia Sh. Bilioni 1.6 kukarabati shule mbili alizosoma Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Enzi za uhai wake Mwalimu Nyerere alianza kupata elimu yake kwenye shule ya Mwisenge kabla ya kuhamia shule ya Tabora baada ya kufaulu vizuri mtihani wa darasa la nne akiwa darasa la tatu.

Ukarabati wa shule hizo unasimamiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na shule nyingine kongwe za Serikali na vyuo vya elimu ya juu.

Kwa nyakati tofauti wakuu wa shule alizosoma Mwalimu Nyerere walimshukuru Rais John Magufuli kwa kuona umuhimu wa kuiishi ndoto ya Mwalimu Nyerere ya kuhakikisha kila mtanzania anapata elimu itakayomsaidia kuondokana na adui ujinga.

Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Mwisenge B, Jones Lumbe, aliwaeleza waandishi wa habari waliotembelea shule hiyo katika kuenzi safari ya kielimu ya Hayati baba wa taifa, Mwalimu Nyerere kwamba Rais Magufuli, amerejesha heshma ya shule hiyo.

"Alipokuja hapa na msafara wake hakutoa taarifa akakuta hali ya Majengo na mazingira kwa ujumla yakiwa chakavu na mengine yalikuwa hayatimiki.

"...Alisema atamuagiza Waziri wa Elimu Profesa Ndalichako aje kufanya tathimini na kuanza maboresho, haikuchukua muda kazi ilianza Aprili29 mwaka huu na itamalizika mwanzoni mwa Novemba.

"Zahanati ya shule imeboreshwa, bwalo la chakula limeongezwa, bweni la zamani limekarabatiwa na kujengwa jingine jipya, madarasa 29 yameboreshwa, nyumba tatu za walimu zimejengwa.

"Ukarabati huu umehusisha pia uwekaji wa umeme, malumalu, jipsam na uzio kuzunguka shule yetu yaani tumepata shule mpya hii itatuongezea morari ya kufundisha," alisema Mwalimu Lumbe.

Mkuu wa shule ya sekondari Tabora, Deograsias Mwambuzi, alisema shule hiyo imejengewa maktaba mpya yenye maandiko mengi yaMwalimu Nyerere, vyumba 17 vya madarasa, matundu mapya 15 ya vyoo, ofisi 10 za walimu na mfumo wa kuondoa maji taka," alisema Mwalimu Mwambuzi.

Akizungumzia ukarabati huo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Ndalichako alisema lengo ni kuitunza historia ya Mwalimu Nyerere hasa upande wa elimu.

"Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuboresha elimu Tanzania ndio maana tulianza na elimu bure, tunaendelea kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifinzaji ili siku moja elimu yetu iwe bora duniani," alisisitiza Profesa Ndalichako.

No comments:

Post a Comment

Pages