HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 16, 2019

Wanaoboronga miradi ya elimu wamchefua Waziri Ndalichako

 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako (wa tatu kutoka kushoto), akikagua moja ya nyumba za walimu katika Shule ya Msingi Kasumo iliyoko wilayani Buhigwe mkoani Kigoma
 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akitoa maelekezo  mara baada ya kukagua ujenzi wa mabweni ya shule sekondari Muyama iliyoko wilayani Buhigwe mkoani Kigoma
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akionesha dosari kwenye jengo la maabara la shule ya sekondari Janda wakati akikagua miradi ya elimu inayotekelezwa katika shule hiyo.
 

Na Mwandishi Wetu, Kigoma

USIMAMIZI mbovu na udanganyifu kwenye miradi ya elimu imemchefua Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako na kutaka wataalam waikague miradi hiyo.

Katika kutekeleza hilo, Profesa Ndalichako alimuahiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Leonard Akwilapo kupeleka wataalam watakaofanya ukaguzi maalum wa utekelezaji wa miradi ya elimu katika Halmashauri ya Wilaya Buhigwe, mkoani Kigoma.

Kauli ya Waziri Ndalichako ilitoka juzi baada ya kukagua baadhi ya  miradi ya elimu inayotekelezwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia chini ya Mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) na kubaini uwepo wa kasoro kadhaa ikiwemo matumizi ya vifaa vya ujenzi vilivyo chini ya kiwango na  majengo ya shule ya Msingi Bwega  kutofautiana na ramani iliyopendekezwa na wizara.

"Kwa ujumla usimamizi wa miradi katika wilaya ya Buhigwe  siyo mzuri, maofisa elimu hawawajibiki katika kuangalia kazi zao, unakuta kazi zimefanyika hovyo, watu hawafuatilii," alisema Waziri Ndalichako.

Alisema Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe hatimizi wajibu wake ipasavyo kwa kuwa ameshindwa kusimamia miradi hiyo kwa viwango vinavyotakiwa na kuruhusu matumizi ya vifaa vya ujenzi visivyo na ubora lakini pia ameshindwa kufuata ramani ya ujenzi wa majengo ya shule ya msingi ya mfano inayojengwa wilayani humo.

Kwa mujibu wa Waziri Ndalichako, amewasiliana na Dk. Akwilapo ili ufanyike ukaguzi wa kina katika miradi ya elimu  wilayani Buhigwe na kubaini dosari zilizosababishwa na uzembe kisha kumuwajibisha aliyehusika.

"Inabidi kabla ya kuleta fedha nyingine za miradi ya elimu wilayani Buhigwe ije timu ya watalaamu mainjinia wachunguze walinganishe BoQ na kilichofanyika, haiwezekani turuhusu uzembe kama huu kuendelea kwenye miradi inayotumia fedha ya wananchi wanyonge," aliongeza Waziri Ndalichako.

Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayanalina, alimshukuru Waziri Ndalichako na kusema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo imetoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri na kwamba zoezi linaloendelea ni kuwachukulia hatua wahusika.

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Anosta Nyamoga alisema ofisi yake imemfukuza kazi fundi aliyekuwa na mkataba wa kukarabati na kujenga vyumba vya madarasa katika Shule ya Sekondari Janda kutokana na kufanya kazi hiyo chini ya viwango na kuahidi kuzifanyia kazi kasoro zote zimebainishwa na Waziri Ndalichako.

Akiwa wilayani Buhigwe Waziri Ndalichako alikagua miradi ya elimu katika shule za msingi Bwega na Kusoma.

Pia alitembelea shule za sekondari Janda na Muyama ambayo jumla ya Sh. Bilioni moja zitatumika kugharamia ukarabati wa shule hizo. 

No comments:

Post a Comment

Pages