WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amekagua ofisi za muda za Halmashauri ya Mtama na kusema ameridhika na
maandalizi aliyoyakuta.
Ametoa kauli
hiyo leo mchana (Alhamisi, Oktoba 17, 2019) wakati akizungumza na watumishi na
madiwani wa Halmashauri hiyo pamoja na wazee wa kijiji cha Mtama kwenye ukumbi
wa mikutano jirani na ofisi ya mbunge wa jimbo la Mtama.
"Nimeridhika
na jitihada zenu za kuja kuandaa ofisi na kufanya usafi ili kutekeleza agizo la
Mheshimiwa Rais. Lakini pia nimefarijika na uamuzi wenu wa kujitolea eneo la
ekari 100 la kujenga Halmashauri yenu," amesema.
Amewataka
watumishi hao wahamasishe ujenzi wa nyumba bora na kuhimiza usafi kwenye makazi
ya watu ili mji wao uendane na hadhi ya makao makuu ya wilaya.
Hamasisheni
ujenzi wa nyumba bora ili pawe na nyumba zenye muonekano wa Halmashauri mpya.
Lakini Bwana Afya simamia usafi kuanzia stendi kule.
Halmashauri
sasa pimeni viwanja. Pato la ndani la Halmashauri yenu mtalipata kwa kupima
viwanja sababu vinauzika. Lazimapawe na mpangilio wa makazi, majengo kadhaa na
maeneo ya biashara," amesisitiza.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amemwagiza Katibu Tawala wa Wilaya ya Lindi, Bw. Thomas
Safari asimamie vizuri fedha za wilaya hiyo ili baadhi ya watumishi wasifuje
fedha za Halmashauri.
"Hakikisha
watu hawatumii fursa hii kufuja fedha za Halmashauri. Hamisha fenicha watu
waanze kazi hapa. Tunahamisha Halmashauri kuja hapa, watumishi msilale Lindi,
bali mlale Mtama."
Naye Mbunge
wa Mtama, Bw. Nape Nnauye alimweleza Waziri Mkuu kwamba tangu Mheshimiwa Rais
Dkt. John Magufuli atoe agizo la kuhamishia makao makuu ya Halmashauri ya Mtama
hapo Mtama, wamekuwa na vikao mbalimbali
na wamefanikiwa kupata ekari 100 ambazo wananchi wamejitolea bure.
"Tumekuwa
na vikao mbalimbali na jioni tutakuwa na kikao na wazee wa hapa ili kuwajulisha
mchakato mzima. Kesho tutakuwa na mkutano mkubwa na wananchi. Lengo letu ni
kuhakikisha tunapunguza gharama kwa kiasi kikubwa," alisema.
No comments:
Post a Comment