HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 18, 2019

CRDB YANOGESHA MAONESHO YA VIWANDA MKOANI PWANI

Na John Marwa

BENKI ya CRDB imenogesha Maonesho ya Viwanda na Uwekezaji ya Mkoa wa Pwani yaliyozinduliwa rasmi na Naibu Waziri wa Viwanda na Uwekezaji Mhandisi Stela Manyanya kwa niaba ya Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu.

Ni mwaka ya pili kufanyika maonesho hayo ambayo yalizinduliwa mwaka jana na CRDB kuwa wadhamini wakuu kwa miaka yote miwili.

Licha ya kuwa wadhamini wakuu wa maonyesho hayo CRDB imekita mizizi katika kusaidia na kuwezesha sekta ya Viwanda katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli, kufikia Tanzania ya uchumi wa kati ifikapo 2025.

Akizungumza katika hotuba yake Mhandisi Manyanya aliipongeza benki hiyo kwa jinsi ambavyo imekuwa mstali wa mbele katika kuwezesha sekta ya viwanda kupitia makampuni na wawekezaji wakubwa kwa wadogo waliojikita katika kuanzisha na kuendeleza viwanda nchini.

“Kwa dhati niwapongeze kwa kuweza kuwa wadhamini wakuu kwa mwaka wa pili mfululizo katika maonesho haya, pili Serikali inatambua na kuthamini kazi nzuri mnayoifanya kwenye sekta ya viwanda na uwekezaji katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano, kuelekea kwenye Tanzania ya Uchumi wa kati.

“Imani yetu ni kuona mnaendelea kuwa sehemu mapinduzi makubwa ya Tanzania ya Viwanda na Uwekezaji. Hongereni sana, naamini hata katika maonesho yajayo mtaendelea kuwa wadhamini wakuu, alisema Manyanya.

Kwa upande wa wadhamini wakuu wa maonesho hayo benki ya CRDB, Mkurugenzi mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela aliyewakilishwa na kaimu mkurugenzi wa idara ya wateja wakubwa, Prosper Nambaya katika hafla hiyo  ya uzinduzi wa wiki ya maonesho hayo ameeleza kuwa benki hiyo imefanikiwa kuongeza mtandao wake kuweza kufikisha huduma kwa urahisi zaidi.

“Benki hii ya CRDB ni benki kubwa kabisa ya kizalendo inayoongoza katika amana, rasilimali na mikopo hapa nchini. Kwa sasa Benki ya CRDB inafanya kazi katika mwamvuli wa kampuni tanzu mbili: “CRDB Bank-Burundi” ambayo imefunguliwa nchini Burundi ili kujenga daraja la kibiashara kati ya nchi hizi mbili.  “CRDB Insurance and Brokerage Ltd” inayotoa huduma za bima na udalali.

“Benki ya CRDB imefanikiwa kukua na kuongeza mtandao wake hivyo kuweza kufikisha huduma muhimu za fedha kwa watanzania wengi zaidi, hususani wa vijijini. Kwa sasa Benki ya CRDB ina mtandao matawi 252 yaliyosambaa nchi nzima pamoja na: Matawi yanayotembea (Mobile branches 13), Mashine za kutolea fedha (ATMs) 525, Kaunta maalum 67 za huduma kupitia shirika la Posta, Mawakala zaidi ya 10,000, Huduma kupitia simu za mikononi yaani “SimBanking” na Huduma kupitia mtandao wa internet yaani “Internet banking”. Amesema Nambaya na kubainisha kuwa.

“Leo tunajivunia sana kuweza kuendelea kuwa wadhamini wa Maonesho haya ya viwanda hapa Kibaha. Huu ni mwaka wa pili mfululizo tumekuwa wadhamini wakuu wa maonesho haya.

“Adhma yetu ni kuendelea kuunga mkono kwa vitendo, juhudi za Serikali yetu ya awamu ya tano, chini ya uongozi wa Raisi wetu mpendwa, Mheshimiwa Dokta John Pombe Magufuli ya kujenga Tanzania mpya, yenye uchumi unaoshamirishwa na viwanda. Pia Nambaya ameweka bayana juu ya jukumu lao la msingi.

“Moja ya jukumu kubwa la Benki ya CRDB ni kutoa mikopo kwa wateja wake. Tukiwa Benki ya kizalendo tunajivunia sana kuwa benki iliyotoa mikopo mingi zaidi kwa watanzania kuliko benki zote nchini.

Tumekuwa sehemu kubwa ya mafanikio ya ukuaji uchumi kwa kugusa sekta zote za uchumi ikiwemo Miundo-Mbinu, Ujenzi, Usafirishaji, Kilimo, Utalii, Viwanda na kadhalika. Kwa kipindi cha mwaka jana 2018 pekee, benki ya CRDB ilitoa jumla ya mikopo yenye thamani ya shilingi trilioni 2.89.” Nambaya hakuishia hapo amebainisha kuwa.

“Tunatambua kuwa ili adhama ya kujenga viwanda ifikiwe, baadhi ni lazima pia tuboreshe sekta ya kilimo. Benki ya CRDB inatoa mikopo mingi sana katika sekta ya kilimo nchini kupitia makampuni, wakulima binafsi, AMCOS na Vyama vya Ushirika katika mazao ya kimkakati ya pamba, korosho, katani, kahawa, kokoa, chai, tumbaku na miwa, ambayo ndiyo malighafi kubwa ya viwanda vyetu.

“Kwa mwaka jana pekee, benki ya CRDB ilitoa mikopo ya zaidi ya shilingi bilioni 433.5 katika kilimo, ambayo ni asilimia 15 ya mikopo yote iliyotolewa. Pia Benki imetoa mikopo ya zaidi ya shilingi bilioni 57.8 katika biashara na usafirishaji ili kurahisha kufikia masoko. Na kuongeza kuwa.

“Mbali na uwezeshaji tunaofanya kupitia huduma za mikopo, Benki ya CRDB pia inatoa huduma nyengine mbalimbali ambazo zinawapa wateja wetu urahisi, unafuu na kuweka mazingira mazuri ya uendeshaji wa biashara zao, baadhi ya huduma hizo ni pamoja na; Dhamana za Biashara (Trade Finance), Huduma za Bima, Huduma za Hazina (Fedha za kigeni), Akaundi ya Hundi maalum kwa biashara, Madawati maalum ya biashara za China na India.

“Katika maonyesho haya ya mwaka huu, Benki ya CRDB kauli mbiu yetu ni “Tupo Tayari na Ulipo-Tupo”, ikimaanisha kuwa: Tupo tayari kutoa mikopo kwa wawekezaji katika sekta ya Viwanda ili kusaidia juhudi za serikali katika kukuza uchumi wa nchi yetu.

Maonesho hayo yanafanyika Wilayani Kibaha Mkoani huyo huku yakirtarajiwa kudumu kwa siku saba ambapo yatatamatishwa Oktoba 23 mwaka huu.
 
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya, akiwasili katika maonesho ya pili ya Viwanda na Biashara mkoani Pwani huku akiongopzana na Mkuu wa mkoa huo. Maonesho hayo yamedhaminiwa na Benki ya CRDB.
 Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya, akiwa katika banda la Benki ya CRDB.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya, akisaini kitabu cha kumbukumbu katika banda la Benki ya CRDB. Kushoto ni Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa Benki ya CRDB, Prosper Nambaya.
  Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya, akifurahia jambo na Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa Benki ya CRDB, Prosper Nambaya.
 Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya, akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa Benki ya CRDB, Prosper Nambaya (wa pili kushoto), wakati wa uzinduzi wa Maonesho ya Viwanda na Biashara mkoani Pwani jana, Benki ya CRDB ni wadhamini wakuu wa maonesho hayo.
 Meza Kuu.
 Baadhi ya wafanyakazi wa Benki ya CRDB wakiwa katika maonesho hayo.
 Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa Benki ya CRDB, Prosper Nambaya, akitoa hotuba yake wakati uzinduzi wa Maonesho ya Viwanda na Biashara mkoani Pwani ambapo Benki ya CRDB ni wadhamini Wakuu wa Maonesho hayo.
 Wafanyakazi wa Benki ya CRDB wakiwa katika picha ya pamoja.

No comments:

Post a Comment

Pages