November 22, 2019

Agizo la Rais Dkt. John Pombe Magufuli latekelezwa kwa asilimia 100 Sumbawanga

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (katikati waliokaa), akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga pamoja na viongozi wengine. 

 Na Mwandishi Wetu

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo, amewapongeza madiwani pamoja na watumishi wa halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kwa kuweza kutekeleza agizo la Rais Dkt. John Pombe Magufuli alilolitoa tarehe 6, Oktoba 2019 alipokuwa katika ziara yake ya siku 3 ambapo aliiagiza halmashauri hiyo kuhamia Laela pamoja na halmashauri nyingine nchini kuhamia katika maeneo yao ya kiutawala.
Amesema kuwa ni watumishi 16 tu kati ya watumishi 165 wa makao makuu ya halmashauri wanaotumia mifumo ya watumishi (LAWSON), mfumo wa mapato LGRCIS), Mfumo wa malipo wa EPICOR, TASAF na Kitengo cha Uchaguzi ndio waliobaki mjini wakisubiri miundombinu hiyo kukamilika katika makao mapya ya halmashauri hiyo katika Mamlaka ya mji mdogo wa Laela.
“Nitoe maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kushirikiana na Wadau wengine (Mfano TTCL) ahakikishe anaunganisha Makao Makuu Mapya ya Halmashauri Laela kwenye Mkongo wa Taifa.  Hii itawezesha Mifumo mingine inayotumia Mtandao wa mawasiliano kuweza kufanya kazi kutokea hapa hapa Laela.  Ninamuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha Watumishi ambao bado hawajahamia Laela wawe wamehamia ifikapo tarehe 1 Januari, 2020.” Alisema.
Aidha, ameitaka menejimenti ya halmashauri hiyo kwa kushirikiana na wadau kufanya tathmini juu ya kuwafikia wananchi waliopo mbali na Laela kama vile kutoka katika vijiji vya mfinga, Mwadui, Kalumbaleza wanaokwenda kupata huduma Laela ambao wanatoka umbali wa zaidi ya kilometa 150.
Ameyasema hayo katika kikao cha baraza la madiwani la kwanza kufanyika katika makao makuu hayo mapya ya halmashauri hiyo tarehe 21.11.2019, kikao kilichohudhuriwa na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa, madiwani pamoja na watumishi wa halmashauri.
Awali akitoa taarifa ya maandalizi ya kuhamia katika makao hayo mapya Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule alisema kuwa kitengo cha uchaguzi kimebaki mjini kutokana na kukosekana kwa eneo kubwa la kuhifadhia vifaa vya uchaguzi lakini mara tu uchaguzi utakapopita kitengo hicho kitahamia katika mji wa Laela.
“Kwahiyo Wakimaliza uchaguzi wakiandaa ile taarifa tutahakikisha nao wanahamia haa Laela, Watu wa Fedha na watu wa Utumishi wanawasiliana na watu wa TTCL ili mokongo ule wa taifa uweze kupatikana hapa Laela na zile huduma zao ziweze kuhamia hapa Laela, kwa ujumla shughuli zinaenda vizuri na wananchi wanaendelea kuhudumiwa vizuri hapa Laela,” Alisema.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Apolinari Macheta alisema kuwa watumishi wa halmashauri hiyo walikuwa wakishiriki usafi wa Jumamosi ya mwisho wa mwezi katika eneo ambalo halikuwa la kwao na pia walikuwa wakichangia maendeleo katika maeneo ambao sio ya kwao.
“Tulichelewa sana na ni maamuzi ambayo yangefanyika hata huko nyuma tungeweza kuwa parefu zaidi lakini tunakushukuru sana kwa namna mji wetu wa Laela ulivyo hautofautiani na mji wa sumbawanga na hata kama ni changamoto ni za kawaida haziwezi kufanana na za wengine kwakweli tunaonekana tuko mjini.” Alisema.
Wakati akitoa neno la Shukurani mbunge wa jimbo la Kwela Mh. Ignus Malocha alisema kuwa yeye ndio wa kwanza kutangulia kwani ofisi yake ilikuwa ya kwanza kabla ya Mkurugenzi kuhamia katika mji huo baada ya wiki mbili tu tangu Rais Dkt. John Pombe Magufuli kutoa agizo hilo, hivyo alimshukuru mkuu wa mkoa kwa kusimamia zoezi hilo la utekelezaji wa agizo la Rais.

No comments:

Post a Comment

Pages