November 22, 2019

WAZIRI SIMBACHAWENE, KALEMANI KUPAMBA MAONESHO YA KITAIFA YA NISHATI JADIDIFU

Mhandisi Prosper Magali
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), George Simbachawene na Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani, watapamba maonesho ya Siku ya Kitaifa ya Nishati Jadidifu Tanzania yanayoanza Ijumaa Novemba 29, mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Uchunguzi umebaini kuwa, maonesho hayo yanaandaliwa na Jumuiya ya Wadau wa Nishati Jadidifu Tanzania (TAREA) kwa ufadhili wa taasisi za Kingdom of The Netherland, Energy Plus, Brac, Chloride Solar, Solar Sister na Ewura. TAREA ni jumuiya yenye wanachama zaidi ya 796.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa TAREA ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maonesho hayo, Mhandisi Prosper Magali (pichani), amesema maonesho hayo yatafanyika Ijumaa Novemba 29 na Jumamosi Novemba 30, mwaka huu katika Viwanja ya Mnazimmoja jijini Dar es Salaam.

“Maonesho yatafunguliwa Ijumaa na Waziri mwenye dhamana ya Mazingira, George Simbachawene na kufungwa Jumamosi na Waziri wa Nishati, Dk Kalemani atakayemwakilisha Waziri Mkuu,” alisema Magali na kuongeza: “Wadau na watu mbalimbali wajitokeze kwa wingi kushuhudia teknolojia ya renewable energy (nishati jadidifu) kwa kuwa licha ya mambo mengi mazuri yatakayofanyika na kuoneshwa, hakuna kiingilio.”

Aidha, Mhandisi Magali alisema lengo la Maonesho hayo yenye kaulimbi isemayo: “NISHATI JADIDIFU KUFIKIA TANZANIA YA VIWANDA,” ni kuionesha jamii namna Nishati Jadidifu inavyoweza kuchangia maendeleo ya Tanzania kuelekea uchumi wa viwanda ifikapo Mwaka 2025.

“Maonesho yatahusisha Teknolojia ya Nishati Jadidifu, Kutembelea Maeneo Yanayotumia Nishati Jadidifu kuona teknolojia hii inavyofanya kazi, pamoja na warsha na majadiliano ya kitaalamu,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages