November 27, 2019

BENKI YA BIASHARA NA MAENDELEO MASHARIKI NA KUSINI MWA AFRIKA YALETA NEEMA KWA WAFANYABISHARA WA TANZANIA

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Bw. Edwin Rutageruka akizungumza wakati wa mkutano kati ya Benki ya Biashara na Maendeleo Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB) na Wafanyabiashara na Wasafirishaji wa mazao ya biashara nje ya nchi (hawapo pichani) Jijini Dar es Salaam.
 
  
Na Josephine Majura, Dar es Salaam

Benki ya Biashara na Maendeleo Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB), imeahidi neema kwa Wafanyabiashara nchini kwa kuwapatia mikopo nafuu itakayowawezesha kusafirisha na kuuza bidhaa za kilimo nje ya nchi

Hayo yameelezwa na Mwakilishi wa Rais wa Benki ya Biashara na Maendeleo Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB), Bw. Lloyd Muposhi, wakati ujumbe wa Benki hiyo uliopo nchini kwa ziara ya kikazi, ulipokutana na kufanya mazungumzo na Wafanyabiashara wanaojihusisha na uuzaji wa mazao hayo nje ya nchi ikiwemo nafaka, chai, kahawa na katani.

Bw. Muposhi, ameeleza kuwa mazungumzo kati ya pande hizo mbili yalikua mazuri yenye kujenga ambapo kwa mwaka ujao wa fedha ameahidi benki hiyo itawawezesha wafanyabishara ama sekta binafsi kimtaji ili waweze kukuza mitaji yao na kufanya biashara ya ushindani na yenye tija.

Kwa upande wake Mkurenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Bw. Edwin Rutageruka ameishukuru Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuratibu mkutano huo na kuwakutanisha Wafanyabiashara na Uongozi wa Benki ya Biashara na Maendeleo ambapo wamepata muda wakubadilishana uzoefu na kujadili mambo mbalimbali zikiwemo changamoto mbalimbali zinazokabili usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi, uzoefu wa kufanya biashara pamoja na ukosefu wa mitaji.

Bw. Edwin alisema changamoto kubwa iliyopo kwa Wafanyabiashara wa ndani ni ukosefu wa mitaji kwa kuwa ni gharama kubwa kusafirisha bidhaa kwenda nje ya nchi hivyo iwapo TDB wataanza kutoa ufadhili kwa Wafanyabiashara wa Tanzania watakuwa wamewasaidia sana kuondokana na tatizo hilo.

Naye mmoja wa Wafanyabiashara walioshiriki katika mkutano huo Mkurugenzi wa ALASKATANZANIA, Bi. Jennifer Bash ameipongeza Serikali kwa kuandaa mkutano huo kwani umetoa fursa ya kubadilishana uzoefu kati ya Wafanyabiashara hao na uongozi wa benki hiyo.

Alieleza kuwa changamoto kubwa inayowakabili Wafanyabiashara wengi ni uhaba wa fedha na mitaji hivyo mkutano huo umetoa mwanga kwao kwa kuwa wamezungumza mambo mengi ambayo iwapo yatatekelezwa yatapunguza ombwe lililopo la ufanisi wa biashara kwa wafanyabiashara wengi.

Mkutano huo umefanyika Dar es Salaam ambapo ulihusisha Uongozi kutoka Benki ya Biashara na Maendeleo Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB), Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango na Wataalamu kutoka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE).

No comments:

Post a Comment

Pages